Patanisho: Jamaa atembelewa na mke wa rafiki yake masaa 6 mkewe akiwa sokoni

Bett alisema tetesi za yeye kujihusisha kimapenzi na mke wa Ruto zilifanya ndoa ya rafiki huyo wake kuvunjika.

Muhtasari

•Bett alisema kuwa uhusiano wake na Ruto ulidhoofika mwaka wa 2021 kufuatia fitina kwamba alikuwa akitoka kimapenzi na mke wake.

•Bett alibainisha kwamba moyo wake unahangaika baada ya kukosana na rafiki huyo wake wa muda mrefu miaka miwili iliyopita.

Image: RADIO JAMBO

Timothy Bett ,38, kutoka Nandi aliomba kupatanishwa na rafiki yake Hillary Ruto ,36, ambaye alikosana naye takriban miaka miwili iliyopita.

Bett alisema kuwa uhusiano wake na Ruto ulidhoofika mwaka wa 2021 kufuatia fitina kwamba alikuwa akitoka kimapenzi na mke wake.

Alisema kwamba uvumi wa uongo wa yeye kujihusisha kimapenzi na mke wa Ruto ulifanya ndoa ya rafiki huyo wake kuvunjika.

"Alinishuku nafanya urafiki na mke wake lakini haikuwa hivyo. Mke wake alinitembelea siku moja akachelewa.  Alikuja mwendo wa saa nne asubuhi kisha akakaa mpaka saa kitu  kumi jioni. Hakukuwa na mambo mabaya, ni vile tu mgeni akijaa mnakaa tu kupika chai, mambo kama hayo. Mama yangu alikuwa nyumbani. Alipika chakula akatupatia, tukakula alafu saa kumi akarudi kwake," Bett alisimulia.

Aliendelea, "Kulikuwa na fitina ya watu eti niko na bibi yake zikafanya mpaka wakaachana. Nilipojaribu kumtafuta huyo jamaa, alikuwa na hasira mpaka akanitafuta na kisu. Tumetoka mbali sana na huyo jamaa. Hatujazungumza na yeye kwa hiyo miaka miwili imepita. Aliachana na mke wake hadi wa leo."

Ruto alipopigiwa simu alizungumza kisha kukata simu kabla ya Bett kujitetea kuhusu madai ya kuwa na mahusiano na mke wake.

Bett alisisitiza kwamba hakuna chochote kibaya ambacho kilifanyika wakati wa ziara ya mkewe Ruto nyumbani kwake.

"Ningetaka kuomba msamaha kwa yale yalitokea. Hatujazungumza miaka miwili. Fitina ya watu haisaidii lakini haikuwa hivyo," Bett alisema.

Alisema zaidi, "Hakuna kitu nimeficha ni ukweli. Mke wangu alikuwa ameenda kwa soko. Nilimueleza mke wangu. Ilikuwa mchana."

Bett alibainisha kwamba moyo wake unahangaika baada ya kukosana na rafiki huyo wake wa muda mrefu miaka miwili iliyopita.

Alidai kwamba alidhani Ruto alikuwa amemruhusu mke wake kumtembelea ila akaweka wazi yeye hakuwasiliana naye. 

"Nitajaribu kumtafuta. Huyo jamaa tumetoka na yeye mbali. Sijiskii vizuri kukosana na huyo jamaa.. Nafikiri (mkewe Ruto)  alikuwa ameomba ruhusa," Bett alisema.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza na Ruto hewani, Bett alisema, "Bw Hillary tumetoka mbali na wewe na ningependa tuendelee kuishi hivyo hivyo. Hakuna ambacho kilifanyika."

Je, una maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?