Patanisho: Jamaa asimulia jinsi uraibu wa betting ulivunja ndoa yake ya miaka 3

Newton alidai kuwa baada ya mkewe kumuacha alitafuta mtumishi wa Mungu ambaye alimuombea na kumsaidia kukabiliana na uraibu wake.

Muhtasari

•Newton alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitatu baada ya yeye kushindwa kukabiliana na uraibu wa kamari.

•Newton alisema amekuwa akiwasiliana na mzazi huyo mwenzake licha ya kukosana ila wakati mwingine amekuwa akimblock.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Newton Etuku ,26, kutoka Donholm alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Rehema Hamisi ,23, ambaye alikosana naye takriban miezi miwili iliyopita.

Newton alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitatu baada ya yeye kushindwa kukabiliana na uraibu wa kamari.

"Nilikuwa mraibu wa betting kidogo. Kuna mengi yalifanyika. Nilikuwa nimeacha kama mwaka moja sikuwa nabet. Baadaye uraibu ukarudi, kazi yangu ilikuwa imekwama kidogo. Nilikuwa nimefungua biashara ya  hoteli lakini haikuwa inafanya vizuri," Newton alisimulia.

Aliendelea, "Mke wangu akawa ananivumilia, alikuwa ananipatia muda nibadilike lakini sikuwa nabadilika. Kama miezi miwili iliyoopita baada  ya kufunga biashara yangu, nilikakaa kwa nyumba nikiwa na msongo wa mawazo ikawa mke wangu ndiye anagharamia mahitaji ya nyumba. Nikarudi kwa betting tena, akaona hawezi kuvumilia akaondoka. Sasa hivi nimeacha kabisa hata naenda kanisa."

Newton alifichua kwamba mkewe alihamia kwa rafiki yake baada ya kushindwa kumvumilia.

Alisema amekuwa akiwasiliana na mzazi huyo mwenzake licha ya kukosana ila wakati mwingine amekuwa akimblock.

"Sasa nahisi nimebadilika. Niliacha mambo ya betting. Nimepata kazi ambayo najishikilia nayo kidogo. Nilipata nyumba ya bei ya chini na imenifungulia njia ya kutafuta kazi naweza kunipatia pesa kidogo," Newton alisema.

Newton alidai kuwa baada ya mkewe kumtema alitafuta mtumishi wa Mungu ambaye alimuombea na kumsaidia kukabiliana na uraibu wake.

Wakati Bi Rehema alipopigiwa simu, Newton alitumia fursa hiyo kuomba msamaha na kumwambia anajuta kumkosea.

"Naomba msamaha kwa yale nilifanya. Nisamehe, sitarudia. Pole sana, urudi nyumbani tujijenge tene. Nakupenda sana," Newton alisema.

Rehema hata hivyo alikata simu kabla ya mpenzi huyo wake kumaliza kuongea.

Newton alisema, "Bado ako na hasira. Wakati mwingine huwa nampigia masaa kama haya na anachukua. Hapendi kuwa exposed. Najuta sana, huwa anasema nimpatie muda. Hata nguo zake bado ziko kwa nyumba.

"Najuta enyewe nilimkosea. Hakuna makosa mengine nimemfanyia isipokuwa hiyo betting. Kuna wakati nilibet na 2,500. Niliwekelea mara mbili 2500 na 2000. Nilikuwa nabet naacha kama miezi mitano tena narudi. Sikuwa nabadilika." Aliongeza.