Patanisho: Mwanadada akataa kumrudia mumewe baada ya kumtishia ameoa ili kumshinikiza arudi

Margaret alifichua kuwa mzazi huyo mwenzake alimwambia tayari ashapata mwanamke mwingine na kumuoa.

Muhtasari

•Brian alisema mkewe alitoroka kufuatia tetesi za majirani ambao walimwambia kuwa mama mkwewe hakumtaka pale nyumbani.

•Brian hata hivyo alikana madai ya kuoana kueleza kuwa alikuwa akimtishia mkewe tu ili akubali kumrudia.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Brian Sirengo ,28, kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mzazi mwenzake Margaret Nyokani ,23, ambaye alikosana naye takriban miaka miwili iliyopita na akagura ndoa yao ya miaka mitano.

Brian alisema mkewe alitoroka kufuatia tetesi za majirani ambao walimwambia kuwa mama mkwewe hakumtaka pale nyumbani.

"Tulikuwa tunaishi na mke wangu vizuri mwaka wa 2021.Kukawa na maneno kidogo ya watu wakaanza kumwambia kuwa mama yangu anamsema vibaya na hamtaki. Basi ikawa hivyo akasema anataka kwenda nyumbani. Nikamuitia motorbike ya kumpeleka nyumbani. Mwenye pikipiki akakataa kumpeleka akasema nimpeleke mwenyewe kwa sababu najua kuendesha. Tukaenda akafika kwao," Brian alisimulia.

Aliendelea, "Baada ya mwezi mmoja nikampigia nikamuuliza kwani harudi akasema harudi. Alisema mama yangu anamuongelea vibaya na ati alisema labda nikae huko kama amekufa. Nilimuuliza mamangu akasema ni maneno ya majirani tu. Margaret alisema nihame nyumbani ili tukae na yeye. Bado sijahama nataka nijue msimamo wake ili nijue kama nitahama."

Brian alikiri kwamba baada ya Margaret kukataa kurudi alimnyang'anya mtoto wao wa miaka mitatu akitumai kwamba mzazi huyo mwenzake angemfuata nyuma na kurudia ndoa yao iliyosambaratika.

Margaret alipopigiwa simu alibainisha kuwa hana nia ya kurudi na kumtaka mume huyo wake wa zamani kuendelea na maisha yake.

Brian alijaribu kumuomba msamaha huku akimshawishi arudi ili waendelee kulea watoto wao wawili pampja.

"Najua nilikosea, naomba uhurumie mtoto. Nilikunyanganya mtoto naomba unisamehe," Brian alisema.

Margaret hata hivyo alifichua kuwa mzazi huyo mwenzake alimwambia tayari ashapata mwanamke mwingine na kumuoa.

"Yeye aliniambia alishaoa na hata anaishi na bibi yake mpya. Amove on na maisha yake. Alichukua mtoto alee tu. Kama atamleta ni sawa," Margaret alisema.

Brian hata hivyo alikana madai ya kuoana kueleza kuwa alikuwa akimtishia mkewe tu ili akubali kumrudia.

Hata hivyo, alikubaliana na uamuzi wa Margaret na kuweka wazi kuwa atamrudhishia mtoto ili aendelee kumlea.

"Siwezi kupinga. Mtoto kulelewa na mzae sio vizuri," alisema.

Aliongeza, "Margret mimi ningependa kukwambia kumbuka mahali tumetoka. Ni mengi yamefanyika. Tulirudiana tukapata mtoto mwingine baada ya kupoteza mwingine hata baada ya watu kusema hatuwezi kurudiana. Nitakuletea Lucky umlee kwa sababu singependa kuskia maneno. Najua utalegeza moyo wako, unisamehe."

Je, una ushauri gani kwa wawili hao?