Patanisho: Mume wangu alitorosha mwanangu kwenda kwa dadake, nikamuitia polisi

“Alikuwa amemficha mwanangu, tulienda na polisi kumchukua mwanangu, nikalala kituo cha polisi halafu kesho yake nikarudi Nakuru na mwanangu,” Diana alisema.

Muhtasari

• Diana alisema kwamba alikwenda mazishi nyumbani kwao Kakamega na baadae mumewe akaanza kumtumia jumbe nyingi za kumkasirisha.

• Alisisitiza kwamba hawezi kurudi kwa mumewe Machakos kwa kile anasema kwamba hasaidii mtoto na kwamba alishaoa mwanamke mwingine.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kippindi cha Asubuhi kwenye Radio Jambo kitengo cha Patanisho na Gidi na Ghost, mrembo Diana Samba mwenye umri wa miaka 25 kutoka Nakuru aliomba kupatanishwa na shemeji yake wa kike ambaye walikosana mwaka 2021.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Bi Diana alisema kuwa shemeji yake Jacinta Kanini alikuwa anaishi na mwanawe baada ya Diana kukosana na baba mtoto wake.

Baadae alikwenda kwa shemeji yake na kuchukua mtoto wake bila kumjuza shemeji yake ambaye kwa sasa yuko Kitui, hatua ambayo ilimkasirisha na kumvimbia.

“Nilikuwa nimeoleka Machakos, tukakosana na bwanangu na akachukua mtoto akapeleka kwa dadake Kitui. Ilifika dakika ya mwisho babake akaacha kumsapoti mtoto ndio mimi nikaamua kwenda kuchukua mtoto lakini sikuambia shemeji yangu. Tulivurugana kidogo lakini nilichukua mtoto wangu…” alisema Diana.

Alisisitiza kwamba hawezi kurudi kwa mumewe Machakos kwa kile anasema kwamba hasaidii mtoto na kwamba alishaoa mwanamke mwingine.

Alisema kwamba anataka kumuomba shemeji yake msamaha kwa sababu wakati wa kuendea mtoto, walivurugana hadi akamfikisha kituo cha polisi.

“Alikuwa amemficha mwanangu, tulienda na polisi kumchukua mwanangu, nikalala kituo cha polisi halafu kesho yake nikarudi Nakuru na mwanangu,” Diana alisema.

Diana alisema kwamba alikwenda mazishi nyumbani kwao Kakamega na baadae mumewe akaanza kumtumia jumbe nyingi za kumkasirisha jambo lililomfanya kutorudi kwa mumewe.

Kwa upande wake Kanini, alisema Diana alikwenda kwao akapata kazi huko huku akimuacha mtoto wake na kakake.

Alisema kuwa Diana alikuwa anakwenda kumuona mtoto na kurudi Nakuru lakini siku moja akamshtukizia akiwa na kisirani akitaka mtoto na hapo ndio zogo lilitokea hadi polisi kuingilia kati.

“Mtoto alikuwa ananipenda sana, nikatoka na mtoto na yeye alitoka akaenda na polisi. Mimi niko hapo kwa kibanda nikaona polisi, nikatoroka mbio. Tukapelekana mpaka kituoni, tukaongea tukasikilizana na nikampa mwanawe na nikakasirika,” Kanini alisema.

Kanini alimtaka Diana kurudi nyumbani kwani yeye ndiye aliachiwa boma ya wazazi wake baada ya kumshughulikia mama wa mume wake aliyekuwa mgonjwa hadi kufariki kwake.

“Mimi nishakusamehe kabisa nimetoa kwa roho. Mimi ni kama mama yako sina ubaya na wewe. Ukitaka kwenda nyumbani uko huru, wewe ndio mama aliachia hiyo boma. Mamangu akifariki tulikuwa na wewe na si alikwambia uchunge boma. Kaa chini ufikirie mimi sina shida na wewe hata kidogo,” Kanini aliwambia Diana.