Patanisho: Jamaa amlilia mkewe arudi baada ya kupatikana na mpango wa kando

"Hadi nimetoa machozi. Saa hii ndio najua umuhimu wake juu hatuko pamoja. Sina amani," Albert alisema.

Muhtasari

•Albert alisema ndoa yake ya miaka mitano ilianza kuyumba baada ya mkewe kumpata na mpango wa kando.

•Sharon alisema, "Nimekusamehe, nimekupea time ufanye kitu unafanya.. Kurudiana sio shida lakini nimempea muda."

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Albert Waswa ,28, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Sharon Wanga,22.

Albert alisema ndoa yake ya miaka mitano ilianza kuyumba baada ya mkewe kumpata na mpango wa kando.

"Tulikuja na mke wangu jijini Nairobi kwa ajili ya kazi. Vile tulikaakaa kidogo akapata kazi ya nyumba akaenda. Huwa anakuja weekend. Kuna msichana alikuwa ametoka nyumbani akakuja kazi. Aliniambia amefukuzwa huko mahali alikuwa anakaa nami nikamwambia akuje akae kidogo alafu aende. Asubuhi bibi yangu akanipigia simu, sikuchukua. Kumbe huyo msichana alichukua namba ya bibi yangu akampigia. Bibi yangu alinipigia baadaye akasema ni heri tuachane," Albert alisimulia.

Aliendelea, "Mke wangu alikuja jana kuchukua nguo zake nikajaribu kumuomba msamaha lakini alikataa kunisikia. Alikuwa amekasirika. Nimeachana na mpango wa kando ata sitaki mambo yake. Hata nilifuta namba yake juu ata anapigia bibi yangu anampatia maneno. Kweli naumia sana, mke wangu nikimpigia anasema hataki kusikia."

Sharon alipopigiwa simu, Albert alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha na kumweleza jinsi anavyojuta makosa yake.

"Enyewe siko sawa. Naomba msamaha. Kila kitu nilifanya nilifanya kwa kutojua. Ukirudi tukae pamoja nitakuheshimu kama mke wangu. Naomba msamaha. Sitarudi tena kukukosea. Naomba tukae chini kama bibi na bwana sitarudi kukukosea. Nimejuta kitu nilikufanyia ni mbaya, sitarudia. Saa hii vile uko huko ndiyo naona kitu nilifanya ni mbaya," Albert alisema.

Sharon alisema, "Nimekusamehe, nimekupea time ufanye kitu unafanya.. Kurudiana sio shida lakini nimempea muda."

Albert alikiri kwamba amenyenyekea hadi kumwaga machozi.

"Hadi nimetoa machozi. Saa hii ndio najua umuhimu wake juu hatuko pamoja. Sina amani," alisema. 

Alimwambia mkewe, "Nataka nimpatie heshima kama mke wangu kwa sababu amenivumilia sana. Ningependa unisamehe, naomba unisamehe. Nitakupea heshima kama mke wangu."

Sharon alisema, "Anipe muda mpaka roho yangu itulie juu amenifanyia vibaya sana. Mchezo ndo sitaki. Aende nyumbani kwetu aongee na mzee wangu."

Je, ushauri wako kwa wawili hao ni upi?