Funguanisho! Jamaa atabasamu baada ya kufunguliwa na ex aliyemwambia hatawahi kuoa mwingine

Moses alidai kuwa anashuku mkewe alimuachia laana ya kutopata mke mwingine baada ya kutengana naye.

Muhtasari

•Moses alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili mwaka wa 2020 baada ya kushuku kuwa ana mipango ya kando.

•Jemila alidai kuwa mpenziwe huyo wa zamani amekuwa na mahusiano na wanawake wengine baada ya wao kutengana.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Moses Wamocho ,28, kutoka kaunti ya Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake, Jemila Shimale (28) ambaye alitengana naye takriban miaka mitatu iliyopita kufuatia kutoaminiana.

Moses alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili mwaka wa 2020 baada ya kushuku kuwa ana mipango ya kando.

Pia alieleza kwamba alikuwa mlevi, tabia ambayo aliweka wazi kuwa sasa  ameacha.

"Nilikosana na mke wangu juu alikuwa ananishuku mambo ya wanawake. Kwa kweli mimi sikuwa na makosa kwa sababu hata niliacha pikipiki nikaenda mambo mengine. Nilifika mahali nikaachana na yeye nikakuja Nairobi," Moses alisema.

Aliendelea, "Tena nilikuwa nakunywa, nilikuwa mlevi, lakini saa hii nimeokoka. Siku hizi nacheza keyboard kwa kanisa. Niliokoka siku hizi sikunywi pombe, kwa kweli nilikuwa natumia kila kitu."

Moses aidha alifichua kuwa anashuku mkewe alimuachia laana ya kutopata mke mwingine baada ya kutengana naye.

"Aliniambia sitawahi oa bibi mwingine, nitaoa wakienda. Nimekuwa nikioa wakienda. Huwa nampigia simu anakata. Saa zingine ananiambia ningoje kidogo, nikingoja hanipigii," alisema.

Jemila alipopigiwa simu alibainisha kuwa hakuwahi kuwa kwenye ndoa na Moses ila walikuwa marafiki tu.

Alidai kuwa mpenziwe huyo wa zamani amekuwa na mahusiano na wanawake wengine baada ya wao kutengana.

"Juzi amepost mwanamke mwingine ameoa kwenye Facebook na WhatsApp.  Alipost mmoja ako na mtoto, namwingine ako na mimba. Kuna mmoja aliweka wakiwa wanaoa kanisani. Juzi amepost mwingine kama ako na mimba," Jemila alisema.

Moses alijitetea, "Mwenye nilikuwa nimeoa ndiye alikuwa ameingia kwenye akaunti yangu ya Facebook akapost. Huyo alienda kwao, alikuwa Mkamba na alirudi kwao.  Mwenye anasema aliona tukiwa kwa kanisa ni dada yangu. Mwenye alienda ndiye alibebaba akaunti yangu hadi line zangu zingine "

Jemila alimshtumu mpenzi huyo wake wa zamani kwa kuhangaika sana na wanawake na kukosa msimamo

"Mimi tuliachana kitambo ata hatujakuwa tukiongea. Familia yake pia iliingilia kati. Mimi simtaki. Kuna mambo mengi alifanya ambayo si mazuri," alisema.

Kufuatia msimamo wa Jemila kuwa hamtaki tena, Moses alimuomba mwanadada huyo amfunge ili mahusiano yake yafanikiwe.

"Juu aliniambia sitawahi kaa na wanawake, nataka anifungue tu sasa. Kuliko naoa tu wakienda. Kuna mmoja tu alienda na mimba yangu," alisema.

Jemila alisema, "Mimi sina shida na yeye kabisa. Sina shida na yeye na namuombea apate msichana mzuri. Atulie na awe mwaminifu awache kuhangaika."

Kwa upande wake Moses alisema , "Kama umeniifungua nashukuru. Nimeshukuru sana, asante kwa kunifungua. Nitatafuta mwenye alienda na mtoto wangu nimuoe."