Patanisho: Mwanadada atoroka baada ya kushambuliwa, kupigwa na shemeji zake wenye miili mikubwa

"Dada zake walinivamia wakanipiga. Wazazi wake wakatuma msichana mwingine akuje awasaidie dada zake kunipiga," Sharleen alilalamika.

Muhtasari

•Sharleen alimtaka mzazi huyo mwenzake kuwatafuta wazazi wake huku akieleza kuwa makosa ambayo alifanya yaliwahusu.

"Walinipiga kwa kunidharau kwa sababu mimi ni mdogo. Wao wako na mwili mkubwa na mimi ni mdogo. Walitaka vitu wanasema nakubalia tu," Sharleen alisema.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Zablon James ,30, kutoka Kakamega alituma ujumbe akitaka kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Sharleen Shikuza ,23, ambaye alitengana naye takriban miaka miwili iliyopita.

Zablon alisema ndoa yake ya miaka 5 ilisambaratika Agosti 2021 wakati mkewe alitoroka baada ya kuzozana naye kuhusu simu.

"Ilikuwa ni maneno ya kuzozana kwa simu na yeye. Nikitoka kazini nilipata anainama tu kwa simu ni kuchat. Nikimuuliza anauliza mbona naingilia mambo yake. Keshoye nikitoka kazini kurudi nyumbani nikapata amechukua virago vyake na ameenda na mtoto. Nikajaribu kufuatilia lakini nikimtafuta nikapata amenifungia simu. Kuulizia mama yake kama amefika nyumbani aliniambia bado," Zablon alisema.

Aliendelea, "Baada ya mwaka mmoja nikaanza kumtafuta tena lakini alikuwa hapatikani. Siku moja alipatikana ila akasema hawezi kurudi kwangu ati mimi huwa nampimia mahewa kwa simu. Vile aliniambia hivyo akaongeza kuwa maisha yangu imembore. Mimi nikamuomba tu arudi akasema hawezi kurudi."

Licha ya mkewe kususia kurudi hapo awali, jamaa huyo alisisitiza angependa Sharleen ampe msimamo wake ili apate mwelekeo.

"Alikuwa ananiambia bado hajapata mtu. Ananiambia tu atakuja lakini hakuji. Anasema nimpe muda afikirie kwanza. Yeye tu ndiye nilikuwa nangoja," alisema.

Sharleen alipopigiwa simu, alimtaka mzazi huyo mwenzake kuwatafuta wazazi wake huku akieleza kuwa makosa ambayo alifanya yaliwahusu.

"Mwambie atafute wazazi wangu. Hakuna vile mimi nitafanya uamuzi na makosa ambayo alifanya inawahusu wazazi. Nilipata mtoto, hata kabla nipone, dada zake wakanivamia wakanipiga. Wazazi wake wakatuma msichana mwingine akuje awasaidie dada zake kunipiga, wakawa watatu. Nilijaribu sana hadi nikatoka. Nilienda kwa polisi nikaandikisha P3 lakini sikuweza kulipa pesa ambazo nilidaiwa," Sharleen alisimulia.

Aliongeza, "Walikuwa wananipiga juu ya Ile tu kudharau mtu kwa sababu mimi ni mdogo. Wao wako na mwili mkubwa na mimi ni mdogo. Walitaka vitu wanasema nakubalia tu. Lazima akuje aeleze wazazi."

Zablon hata hivyo alikana madai ya dada zake kumpiga mkewe na kudai kuwa walikuwa tu wanazozana kidogo nyumbani.

"Hawakuwa wanampiga, walikuwa wanazozana tu kwa nyumba. Alikuwa tu anazozana na ndugu zangu kwa boma," alisema.

Sharleen hata hivyo alisisitiza kuwa dada za mumewe walimpiga hadi akaandikisha taarifa kwa polisi.

Zablon alisema, "Hiyo maneno tuliongea ikaisha. Mimi bado nampenda. Wacha nijipange alafu niende nyumbani kwao tuzungumze na wazazi. Sharon, mimi bado nakupenda, nataka urudi. Uchukue mtoto urudi. Sina ubaya na wewe."