Patanisho:Jamaa ahuzunika baada ya mke aliyefanya harusi rasmi naye kumtoroka baada ya kazi kuisha

Steven alisema alifanya harusi na Mariam 2018, wakajaliwa mtoto mmoja pamoja kabla ya ndoa kusambaratika 2020.

Muhtasari

•Steven alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika mwaka wa 2020 wakati mke wake alimtoroka baada ya kupoteza kazi na kujitosa kwenye ulevi.

•Steven alisema ana wasiwasi kwani mzazi huyo mwenzake hajawahi kumpa talaka baada ya kuondoka ilhali walikuwa wamefunga ndoa rasmi.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Jamaa ambaye aljitambulisha kama Steven Lubasia ,28, kutoka Vihiga alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mariam Hamisi ambaye alimuacha takriban miaka mitatu iliyopita.

Steven alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika mwaka wa 2020 wakati mke wake alimtoroka baada ya kupoteza kazi na kujitosa kwenye ulevi.

Alisema alikuwa amefanya harusi na Mariam mwaka wa 2018 na wakajaliwa na mtoto mmoja pamoja kabla ya ndoa kusambaratika.

"Tulifanya harusi. Nilikuwa nafanya kazi kandarasi ikaisha ikabidi nirudi nyumbani. Aliposikia hivyo alianza wasiwasi tukaanza kukosana. Alisema anaenda kutembea kwao nikasema ni sawa. Nilikaa nyumbani kidogo nikaanza kuwa na stress, nikaanza ulevi. Siku moja nilipata tu ameenda. Hajawahi kurudi," Steven alisema.

Aliongeza, "Najua alienda juu ya kazi. Alinipata kama nakunywa pombe. Ulevi Ilizidi baada ya kupoteza kazi. Ilifika mahali nikaanza kupunguza."

Steven alisema ana wasiwasi kwani mzazi huyo mwenzake hajawahi kumpa talaka baada ya kuondoka ilhali walikuwa wamefunga ndoa rasmi.

"Tulifanya harusi na hata hajawahi kunipa talaka. Huwa namfuatilia. Wakati mwingine huwa ananiambia ameoleka, anasema ako na mtu majuu," alisema.

Alisema zaidi, "Tuliongea na yeye mwezi wa sita. Wakati mwingine nikipiga simu hashiki,akishika askie sauti yangu anakata. Bado sijamfuatilia kwao. Huwa nampigia simu kutaka kujua ako wapi. Siwezi enda kwao kama sijui kama ako."

Kwa bahati mbaya, Steven hakuweza kupatanishwa na Mariam kwani alikata simu kila mara Gidi alipompigia.

Steven alipopewa fursa ya kuzungumza naye hewani alisema, "Mariam wewe nipatie msiamamo kama mambo na talaka basi iishe hivyo."

Je, ushauri wako kwa Steven ni upi?