Patanisho: "Yesu ndiye anasamehe lakini mimi sio Yesu!" Mwanadada akataa kumsamehe mumewe

Cytone alikiri kwamba ni kweli alikuwa anaenda nje ya ndoa ila akabainisha kuwa tayari ameacha tabia hiyo.

Muhtasari

•Cytone alisema kuwa mkewe aligura ndoa yao ya mwaka mmoja baada ya kumshuku kuwa na mipango ya kando.

•Cytone alikiri kwamba kuna meseji mbaya ya matusi ambayo alimtumia mkewe ila akaeleza alichochewa na hasira.

Image: RADIO JAMBO

Jumatano asubuhi, jamaa aliyejitambulisha kama Cytone Asango ,31, kutoka kaunti ya Homa Bay alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Millicent Atieno ,29, ambaye alikosana naye takriban miezi sita iliyopita.

Cytone alisema kuwa mkewe aligura ndoa yao ya mwaka mmoja baada ya kumshuku kuwa na mipango ya kando. Alikiri ni kweli alikuwa anaenda nje ya ndoa ila akabainisha kwamba tayari ameacha tabia hiyo.

"Kuna msichana tulipatana naye kisha tukaingia kwa ndoa lakini hatujafanikiwa kupata mtoto. Ilifika wakati akaanza kunishuku hadi ikatutenganisha. Ni ukweli lakini nimeacha hayo mambo," Cytone alisema.

Aliongeza, "Nilijikuta tu hivyo lakini sio kwa sababu ya kutafuta mtoto. Nimeachana na hayo mambo kabisa. Nikijaribu nimuongeleshe hatuelewani. Ni kama bado anaona sijaacha hayo mambo."

Wakati Millicent alipopigiwa simu, mwanzoni alisita kumsamehe mume wake lakini baada ya mazungumzo kidogo akashusha moyo na kumwagiza afike nyumbani kwao ili washiriki kikao.

"Yesu ndiye anasamehe lakini mimi sio Yesu. Meseji ambayo uliniandikia ata mimi bado niko nayo. Utakuja mwenyewe tutaongea," Milicent alisema.

Cytone alikiri kwamba kuna meseji mbaya ya matusi ambayo alimtumia mkewe ila akaeleza alichochewa na hasira.

"Kuna meseji nilimtumia ya hasira najaribu kumuomba msamaha haskii," alisema.

Alimwambia mkewe, "Mimi bado nakupenda. Naomba uniachie makosa nilifanya na tuendelee vizuri."

Millicent alisema, "Akikuja nitaona vile nitamsamehe. Akuje tu lakini asirudie makosa tena."

Je, ushauri wako ni upi kwa wawili hao?