Jamaa aliyejitambulisha kama Charles Martin Mundia mwenye umri wa miaka 24 kutoka Vihiga alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mama Ronnie ,25, ambaye amekuwa mbali naye kwa miezi miwili.
Charles alisema ingawa bado hawajatengana, mkewe alienda kwa dadake akiwa na ujauzito wa mtoto wao wa kwanza pamoja ila bado hajaweza kurejea miezi miwili baadaye. Alisema mkewe alikuwa mgonjwa wakati aliondoka.
"Alikuwa mgonjwa akasema anaenda kwa dada yake kupata matibabu lakini hajarudi. Tuliongea na yeye hata jana lakini hatukuelewana vizuri. Nikimwambia arudi anasema ningoje, nashangaa atarudi siku gani. Bado hajapona lakini saa hii ako poa kidogo," Charles alisema.
Aliongeza, "Nilimuuliza makosa yangu akasema sina makosa yoyote kwake. Kwao bado sijajitambulisha rasmi lakini tumeongea na mama yake kwa simu. Miezi mbili nimekaa nimengoja harudi."
Wakati Mama Ronnie alipopigiwa simu, alizungumza kwa sauti nyonge, ishara kuwa alikuwa anakabiliana na maumivu.
Alidhihirisha kuwa yupo hospitalini ambapo anaendelea kupokea matibabu na Bw Charles bado hajapiga hatua ya kumtembelea.
"Niko hospitali. Ata yeye (Charles) anajua, anajifanya hanijui. Hajakuja kuniona. Tangu nigonjeke hajakuja kuniona," alisema.
Aliongeza, "Nilikuwa nataka damu ili niongezwe mwili. Bado hajakuja. Ata nimemwambia mara mingi hataki kuja."
Charles alijitetea kwa kusema, "Nauli ya kufika huko ndio sina.Vile alikuwa anagonjeka tulikuwa na yeye."
Watangazaji Gidi na Ghost Mulee walimsuta sana jamaa huyo kwa kutopiga hatua ya kumuona mkewe mgonjwa hospitalini na kumuagiza kufanya vile mara moja kabla hata ya mikakati ya kurudiana kuanza.
Je, una maoni yapi kuhusu Patanisho ya leo?