Patanisho: 'Najuta kumfokea mke wangu kuwa sijamuoa yeye ni mfanyikazi wa mamangu'

Eric alisema kwamba alimtamkia mkewe maneno hayo makali baada ya kurudi nyumbani na kumpata anacheza akishikwa shikwa na kijana mdogo ambaye alikuwa jirani yao.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa jamaa huyo, tamko hilo lilimghadhabisha mkewe na kuondoka hadi leo hii na mtoto wao mmoja.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost kwenye stesheni ya Radio Jambo asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa kwa jina Erick alitaka kupatanishwa na mke wake baada ya kile alisema kwamba alimpata na makosa.

Mwanamume huyo kwa jina Erick alisema kwamba alikosana na mke wake mwaka 2020 baada ya kumkuta alicheza na kijana mdogo kwa njia ambayo haikumfurahisha.

Alisema kwamba baada ya kumuuliza, walifokeana vikali kiasi kwamba Erick anafikia mahali pa kumwambia mke wake, Bridgit kuwa hata bado hajamuoa bali yeye ni kama tu mfanyikazi wa mamake.

Kwa mujibu wa jamaa huyo, tamko hilo lilimghadhabisha mkewe na kuondoka hadi leo hii na mtoto wao mmoja.

“Ilikuwa ni 2020 nilikuwa na Bridgit akakuja nyumbani kujifungua na baadae nikatoka nikaenda Nairobi kutafuta kazi. Lakini baadae nilimpata kuna kijana jirani alikuwa anamshika wakicheza kama watoto, kwa hiyo harakati akaanza kunigombanisha tukagombana, nikamjibu kwa ukali wewe hata sijakuoa wewe ni mfanyikazi wa mamangu, akakasirika akaenda mpaka leo hii,” Erick aliongea kwa majuto.

 Alisema kwamba kutilia msumari moto kwenye kidonda, mke wake hivi majuzi amempelekea mamake Erick mtoto nyumbani na kumuacha huko, jambo ambalo linamtatiza na hivyo kutaka kupatanishwa naye kwa ajili ya kulea yule mtoto.

“Juzi akaleta mtoto kwetu mtoto ako na mama, yeye ako Nairobi, mimi niko Nakuru….. nimemfuatilia mpaka kwa dadake lakini bado sijafaulu, hadi kwa mamake…kama atakubali kurudi niko tayari kuenda kwao nimalize taratibu za kumuoa…” alisema.

Hata hivyo, juhudi za Bridgit kupigiwa simu hazikufua dafu kwani alikataa kupokea simu ya Radio Jambo.

Jamaa huyo alisema kwamba alijuta sana kumtamkia maneno makali mke wake lakini akasema kuwa ni kutokana na hasira huku akimtaka Bridgit kama alikuwa anasikiliza radio basi arudi kwa ajili ya mtoto.

Alimsifia kwamba Bridgit alikuwa ni mchapa kazi sana ambaye wakati mwingine alikuwa anawahi kurauka kwenda shambani akimuacha yeye kitandani.