'Nilisaidia mume wangu kujenga, miaka 11 baadae malipo ni ku'cheat na kutusi wazazi wangu'

"Miaka yote 11 tumekaa na yeye mipango ya kando mingi mingi, akipata pesa hivi anapeleka mahali anapeleka mimi navumilia...aliuza ndume akaenda na hata hakutuachia hata shilingi 50." mama alilia.

Muhtasari

• “Tangu anioe tumekaa na yeye miaka 11 na amenitendea makubwa na sitawahi msamehe milele na milele." mkewe alisema.

Image: RADIO JAMBO

Geofrey Mogire, mwanamume mwenye umri wa makamo alipeleka ombi la kupatanishwa na mke wake kupitia kitengo cha Patanisho kwenye  stesheni ya Radio Jambo, akisema kwamba aliondoka kwenda kazini mbali na nyumbani ghafla bila kumjulisha mke wake, Sera Nyangweso.

Geoffrey alisema kwamba walikuwa wanaishi Nakuru lakini aliondoka bila kumwambia mke wake kuenda Namanga mpakani alipopata kazi ya shamba.

Hatua ya kuondoka pasi na kumjulisha mkewe ilimghadhabisha kiasi kwamba akimpigia simu hachukui na kwa wakati mmoja Geoffrey alipiga simu mkewe akampa ndugu yake ambaye Geoffrey alimpokeza matusi ya nguoni kwa hasira.

“Ilikuwa Janauri mwaka huu, mke wangu tumeonana kwa miaka 10, siku moja nikauza ng’ombe na nilikuwa nataka kuenda kazi Namanga, shida ilitokea nilienda kazi ghafla bila kumuelezea lakini tulikuwa tumenongea hapo mbeleni naenda kazi, sasa tangu hapo hachukui simu, siku moja akampa ndugu yake simu na nilikasirika nikamtukana huyo ndugu yake,” Geoffrey alisema.

Alisema kwamba hivi majuzi alipata ajali na kulazwa hospitalini huko Namanga lakini bado juhudi zake za kumfikia mkewe kwa njia ya simu bado zilifeli.

Alitaka Gidi na Ghost wamsaidie kupatana na mkewe.

“Sijawahi rudi na juzi nilipatwa na ajali nikalazwa hospitali wiki mbili nikimtumia ujjumbe hajibu. Bado niko Namanga…pahali tulikuwa tunaisi alihama akaenda akachukua nyumba nyingine… nilimuoa na watoto 2 wa kiume na tukazaa na yeye mmoja msichana…”

Sera alipopigiwa simu, alisema kwamba huyo mzee wake amemkosea heshima kwa miaka 11 ambapo wamekuwa pamoja kwenye ndoa akisema kwamba kwa wakati mmoja hata aliwahi mtukana babake mzazi matusi ya nguoni.

“Tangu anioe tumekaa na yeye miaka 11 na amenitendea makubwa na sitawahi msamehe milele na milele. Sioni kabisa kama nitamsamehe, mpaka anatusi wazazi wangu…miaka yote tumekaa na yeye mipango ya kando mingi mingi, akipata pesa hivi anapeleka mahali anapeleka mimi navumilia, wakati anaenda aliuza ndume akaenda na hata hakutuachia hata shilingi 50, mimi nimempata kwa loji mara nyingi tu lakini navumilia,” alisema.

“Alitukana mzazi wangu baba mambo mabaya ambayo sitawahi ongea kwa redio, hata tukifanya mila kusamehewa ni ngumu, kwao hakuwa amejenga mimi nikashughulika tukajenga na yeye nyumba halafu arudi aseme turidiane na yeye, mimi naenda kanisa na ni Mkisto, aniache kabisa,” mama Sera alisema.