Patanisho:"Nilimaliza kidato cha 4 na nikaamua kuolewa, mamangu akaninyamazia"

"Baadae tukakosana na mume wangu na sikurudi nyumbani, nilienda Naivasha lakini mama akanifuata na kunirudisha nyumbani kwa lengo la kunirudisha shule lakini mimi nilitaka kurudi kwa mume wangu.”

Muhtasari

• Alisema kwamba walirudiana na mume wake na wako na mtoto mmoja huku yeye akiwa mchuuzi wa matunda na mboga na mume wake akifanya kazi ya dry cleaning.

• Mama Josephine Ngonyo alipopigiwa simu, alisema kwamba anajua njia ya kwenda nyumbani na asimsumbue kwa kumpeleka kwenye Radio.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo kitengo cha Patanisho, mrembo Mercy Wanjiku Wainaina mweney umri wa miaka 24 kutoka Nyandarua alitaka kupatanishwa na mamake, Josephine Ngonyo mwenye miaka 52 baada ya kukosana mwaka 2020.

Mrembo huyo alisema kwamba baada ya kumaliza shule ya sekondari, alioleka wakati mamake alikuwa anataka kuendeleza masomo yake katika chuo anuwai, jambo ambalo lilizua mfarakano mkali baina yao.

“Mimi niliamua kuoleka baada ya kidato cha nne na yeye akaninyamazia, akatuma dadangu akamwambia anataka nirudi niende shule, akanipeleka chuo anuwai 2021 nikasoma muhula mmoja tu nikarudi nyumbani na nikaacha shule. Akaja akanitoa kwa mume wangu na fujo na tukanyamaziana.”

“Nikarudi tena tukapatanishwa na ndugu zangu akisisitiza kwamba lazima nirudi shule ndio tuanze kuzungumza. Baadae tukakosana na mume wangu na sikurudi nyumbani, nilienda Naivasha lakini mama akanifuata na kunirudisha nyumbani kwa lengo la kunirudisha shule lakini mimi nilitaka kurudi kwa mume wangu.”

“Mamangu alikataa hilo lakini mimi nikahepa nyumbani na kurudi kwa mume wangu na tangu hapo tulinyamaziana kabisa na mamangu. Tangu huu mwaka Agosti hata tukikutana kwa njia hatuzungumzi, sasa nataka anisamehe kwa sababu watu hata wananiuliza kwa barabara huyo ni mamako kweli, hiyo kitu inaniudhi,” Wanjiku alisema.

Alisema kwamba walirudiana na mume wake na wako na mtoto mmoja huku yeye akiwa mchuuzi wa matunda na mboga na mume wake akifanya kazi ya dry cleaning.

Lakini alisema kwamba haoni kama kuna uwezekano wa kurudi shule, lakini baada ya Gidi na Ghost kumshawishi, alisema kwamba angependa kurudi shule kujifunza mwenyewe.

Mama Josephine Ngonyo alipopigiwa simu, alisema kwamba anajua njia ya kwenda nyumbani na asimsumbue kwa kumpeleka kwenye Radio.

“Anajua mahali anastahili kuenda sio kwa Radio Jambo, anaogopa kwani niko na risasi ngapi mimi, huo ni unafiki. Na mwambie asinisumbue kwa sababu anajua mahali anastahili kuenda, ujinga wake apelike mbali,” mama alizungumza kwa hasira na kukata simu.