Patanisho: "Anaishi na nyanya! Ako na sugar mama!" Mwanadada amuaibisha mumewe vibaya hewani

Morine alimshtumu mumewe kwa kumpiga na kucheza karata nje ya ndoa mara kwa mara.

Muhtasari

•Katika malalamishi yake, Morine alimshtumu mumewe huyo wa miaka miwili kwa kumpiga na kukanyaga nje ya ndoa mara kwa mara.

"Kuna mwanamke anaitwa Mbinya ako huko Kitegela. Ako na mwingine amepost FB. Ndio maana siku hizi nikimpigia hashiki," Morine alisema

Image: RADIO JAMBO

Mwanadada ambaye alijitambulisha kama Morine Muhonja ,27, kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Elias Kahindi ,30, ambaye alikosana naye takriban miezi saba iliyopita.

Katika malalamishi yake, Morine alimshtumu mumewe huyo wa miaka miwili kwa kumpiga na kukanyaga nje ya ndoa mara kwa mara.

"Alikuwa anakuja kwa nyumba ananipiga. Wakati mwingine alikuwa analala nje, nikimuuliza alikuwa wapi ananipiga. Wakati mwingine nikimpikia chakula alikuwa hataki kula. Hata majirani walikuwa wanajua tunapigana," Morine alisema.

Aliongeza, "Wakati nilirudi kwetu, alinipiga mpaka akanirushia manguo nje. Mimi niko nyumbani na mama yangu. Huwa tunawasiliana wakati mwingine. Wakati mwingine huwa anashika simu yangu anasikiliza alafu anakata simu."

Licha ya masaibu yote yaliyokumba ndoa yake, Morine alibainisha wazi kwamba angependa kurudiana na baba huyo wa mtoto wake.

"Maisha ya sasa ni ngumu nataka tuvumiliane tulee mtoto. Nitavumilia hivyo. Nilikuwa nataka kuvumilia tu juu sipendi kuhanya hanya," alisema.

Bw Kahindi alipopigiwa simu alihoji hatua ya mzazi huyo mwenzake ya kumripoti katika kituo cha polisi na akamkosoa kwa hilo.

Morine alimjibu, "Ulikuwa unanidhulumu, ulikuwa unanichapa na hukuwa unanihudumia."

Bw Kahindi hata hivyo alidai kuwa mkewe alikuwa akidanganya.

"Hiyo miaka tatu mbona hakuwa ananishtaki. Ningependa kuenda nyumbani kwao, Nataka niongee niseme yote ambayo nataka hadi nimalize. Nitaenda huu mwezi tu," alisema Kahindi.

Punde baada ya Bw. Kahindi kumaliza hayo, mkewe alianza kumshtumu kwa kuwa na mpango wa kando, "Kuna mwanamke anaitwa Mbinya ako huko Kitegela. Atakuja aje kuniona na ako na mwingine huko Kitengela? Hiyo kitu inanisumbua sana! Ako na mwingine amepost FB. Ndio maana siku hizi nikimpigia hashiki."

Aliendelea, "Anaishi na nyanya. Ni sugar mama. Bwana yangu akitoka kazi wanaenda kukutana mahali. Kuna wakati nilikutana nao alafu baba mtoto wangu aliponiona akaanza kutembea mbele, lakini nilikuwa nishaona."

Bw Kahindi alisema, "Mimi sasa hata simuelewi, anaongea tu stori za kitambo. Yeye ako na shida. Alinipeleka polisi akaitisha pesa anataka kuachana naye. Ilibidi nitoe pesa."

Wawili hao hawakuweza kupatana kwani Kahindi aliishia kukata simu huku mkewe akiendelea kulalamika hewani.

Je, ushauri wako ni upi kwa wawili hao?