Patanisho: Wapenzi washauirwa baada ya kusikika kuchanganyikiwa kuhusu mwelekeo wa ndoa yao

Philemon alibainisha amekuwa mwaminifu kwa mkewe tangu walipojaliwa mtoto takriban miezi sita iliyopita.

Muhtasari

•Philemon alisema mkewe alitoroka ghafla na kurudi kwao mwezi Novemba ila kulingana naye, hawakuwa wamezozana.

•"Tangu tupate mtoto, sijawahi kuenda kando. Hapo kitambo nilikuwa naenda kando kwa sababu tulikuwa bado tunachumbiana," alisema Philemon.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Philemon Agwambo 26, kutoka Kisumu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Florence Adhiambo ,19, ambaye alitoroka ndoa yao ya mwaka mmoja mwishoni mwa mwaka jana.

Philemon alisema mkewe alitoroka ghafla na kurudi kwao mwezi Novemba ila kulingana naye, hawakuwa wamezozana.

"Ilikuwa mwaka jana. Nilikuwa nimetoka. Kurudi nilipata mama mtoto amerudi kwao. Sikujua alitoka kwa nini," Philemon alisema.

Aliongeza, "Tulikuwa tukikosana mara kwa mara lakini tunasuluhisha mizozo. Huwa tunakosana juu ya mambo ya kushuku shuku. Amekuwa akinishuku eti naenda kando kando."

Philemon hata hivyo alibainisha kuwa amekuwa mwaminifu kabisa kwa mkewe tangu walipojaliwa mtoto takriban miezi sita iliyopita.

"Tangu tupate mtoto, sijawahi kuenda kando. Hapo kitambo nilikuwa naenda kando kwa sababu tulikuwa bado tunachumbiana," alisema.

Aliongeza, "Alifaa arudi Desemba 31, tena akasema atarudi Januari ikianza. Sijui msimamo wake. Mtoto ako na miezi sita. Huwa namshughulikia."

Florence alipopigiwa simu "Hakuna kitu ilitokea. Mimi nilitaka tu kurudi kwetu. Mimi bado napumzika. Huko nyuma alinikosea lakini vile nilitoka hakunikosea. Mwambie mimi napumzika hadi hii mwezi iishe."

Philemon hata hivyo alimsihi mkewe arejee hivi karibuni, ombi ambalo alikubali.

"Niko tayari kuolewa. Niko tayari lakini bado namshuku.Wazazi wangu hawana maneno. Akituma fare nitaenda," Florence alisema.

Philemon alimwambia, "Mimi bado nakupenda na ningependa urudi tulee Clara. Mimi bado nakupenda."

Florence pia alimbainishia mzazi huyo mwenyewe kwamba anampenda.

Gidi na Ghost waligundua jinsi wanandoa hao walivyosikika kuchanganyikiwa kuhusu mwelekeo wa ndoa yao na kufuatia hayo wakawashauri kutafuta ushauri wa ndoa kutoka kwa jamaa zao  ambao wamekomaa.