Raia wa Uganda ambaye alijitambulisha kama Kevin Simeraa ,27, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Miriam Isuku ,28, ambaye pia ni raia wa nchi hiyo jirani.
Kevin ambaye anafanya kazi katika eneo la Kandara, kaunti ya Murang'a alisema ndoa yake ya mwaka mmoja ilisambaratika mwishoni mwa mwaka jana baada ya mkewe kukataa kuenda kuishi naye.
"Mke wangu tumekaa naye mwaka mmoja. Nafanya kazi Muranga, yeye ako Nairobi. Disemba 2023 alisema nimpatie nauli aende kwao. Akiwa kwao alisema nimtumie nauli arudi. Nilimwambia bosi ako mbali atafute nauli nitamrudishia. Alisema kama ni hivyo atafute kazi ingine hatawezana na hiyo," Kevin alisimulia.
Kevin alifichua kwamba mkewe alipinga ombi lake la kuenda kuishi naye Murang'a huku akidai kwamba kuna baridi sana.
"Nilimwambia akuje akasema hapana. Alisema kama nataka niache kazi niende tuishi Nairobi. Anataka niache kazi niende tuishi Nairobi. Nashindwa tutalipa kodi na nini. Anasema Murang'a baridi ni mingi," Kevin alisema.
Aliongeza, "Yeye anafanya kazi ya nyumba. Mimi nalisha nguruwe na ng'ombe. Bado sijaenda kwao. Tulipatana Uganda. Watu wao wananijua sana. Nataka nijue msimamo wake kwani mawazo yangu yote nimempatie yeye."
Juhudi za kuwapatanisha wawili hao hata hivyo iligonga mwamba kwani Miriam hakuweza kupatikana kwa simu.
Kevin ambaye alisikika kusikitika alisema, "Wacha akae. Kama hataki hii baridi, mimi siwezi toka kwa kazi yangu niende Nairobi."
Aliongeza, "Akuje tukae hapa Muranga tuzoee baridi ya Muranga juu ata kwetu kuna baridi nyingi. Nitamnunulia kila kitu anataka."
Je, una maoni yapi kuhusu Patanisho ya leo?