Patanisho: Jamaa alalamikia mkewe kuingia Facebook saa moja asubuhi, atishia kumuua kwa panga

Celestine alifunguka kuhusu jinsi mpenziwe alipotishia kumuua kwa panga baada ya kumpata akizungumza na jamaa wake.

Muhtasari

•Dominic alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilivunjika baada ya kumshambulia mkewe alipogundua alikuwa akizungumza na wanaume wengine kwa simu.

•Celestine alishikilia msimamo wake kwamba hatarudi na kumtaka mpenziwe huyo wake wa zamani aendelee na maisha yake.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Dominic Kilonzo ,27, kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Celestine Naswa ,28, ambaye alitoroka mwezi uliopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Dominic alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilivunjika baada ya kumshambulia mkewe alipogundua alikuwa akizungumza na wanaume wengine kwa simu.

"Niligundua kuwa nikienda kazi kuna wanaume huwa anaongea nao. Nilifuatilia nikajua ni marafiki wake wa kitambo. Nilipomuuliza akasema ni majirani wake tu wa kitambo ambao huwa wanamjulia hali," Dominic alisema.

Aliongeza, "Kuna jamaa anaitwa Kiptoo na Newton ambao nilikuwa nawashuku. Niliona wanaongea kimapenzi. Wakiongea huwa anafuta meseji. Kuna wakati simu yake ilipigwa akazima. Alisema eti ni Carol alikuwa anamdai deni lake. Nilimshika vizuri siku iliyofuata na tukaongea naye. Aliniambia ati alikuwa mpenzi wake wa zamani, eti hajawahi kumwambia alioleka. Tulikuwa katika harakati ya kuoana rasmi, lakini alikuwa anasema napeleka mambo haraka.  Alikuwa anasema kuna dada yake ambaye hajawahi kuoelewa ningoja aolewe. Sijamfuatilia kwa sababu sijui huko. Anasema aende kwao aongee na mamake ndiye atatoa uamuzi wa mwisho."

Celestine alipopigiwa simu alikiri kwamba kuna watu ambao alikuwa anazungumza nao kwa simu.

Hata hivyo, alidai kwamba wengi wao walikuwa wanafamilia wake na marafiki zake wa nyumbani ambao hangekosa kuzungumza nao. Aidha, alilalamika kuwa mpenziwe alikuwa akimkataza kuzungumza nao.

"Hiyo kuongea na watu nilikuwa naongea nao. Hata kuna mwenye nilimpea simu akaongea naye. Siwezi nikakosa kuongea. Kuna boy nilikuwa naongea na yeye lakini akamkataza na akakubali," Celestine alisema.

Aliendelea kufunguka kuhusu jinsi mpenziwe alipotishia kumuua kwa panga baada ya kumpata akizungumza na jamaa wake.

"Kuna siku nilikuwa naongea na jamaa wangu, Akauliza kama ni mwanaume. Akasema tuende ataniambia vizuri. Tulienda kwa nyumba akanishikia panga, akanitishia, akaniambia asiponiua nitauliwa na mtu mwingine. Aliniambia vile ataniua na kunizika.," alisema.

Aliongeza, "Mimi siwezi nikarudi huko tena. Ata nilikuwa nimejificha huko, hakuna mtu wa kwetu. Niliamka tu asubuhi nikamtengenezea chai na nikatoka."

Dominic aliendelea kulalamika, "Nikitoka kwa nyumba huwa  anaingia Facebook asubuhi saa moja. Nilikuwa namwambia kama ni kuingia Facebook aingie mchana."

Celestine hata hivyo alishikilia msimamo wake kwamba hatarudi na kumtaka mpenziwe huyo wake wa zamani aendelee na maisha yake.

"Sirudi, umeharibu. Mimi sirudi. Yeye akae maisha yake na mimi nikae yangu. Niache nikae maisha yangu. Nitapata mume wangu," alisema.

Dominic hakuwa na budi ila tu kukubaliana na uamuzi wa mpenziwe.

Je, ushauri wako ni upi?