Patanisho: "Niliona niziuze tukae bila!"Jamaa auza simu yake na ya mpenziwe ili asiongee na wengine

Wafula alisema hali nyumbani iliimarika hadi wakati mpenziwe alipojuana na jirani ambaye alikuwa anamsaidia na simu yake.

Muhtasari

•Wafula alisema ndoa yao ya mwaka moja ilivunjika kufuatia mizozo ya kinyumbani ambayo ilichangiwa na simu.

•Bi Phanice hata hivyo alipingana na madai ya mpenziwe na kudai kwamba alikuwa na mipango ya kando.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Joseph Wafula ,22, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Phanice Wangila ,23, ambaye alikosana naye mwaka jana.

Wafula alisema ndoa yao ya mwaka moja ilivunjika kufuatia mizozo ya kinyumbani ambayo ilichangiwa na simu.

Alisema mkewe alikuwa na mazoea ya kuomba simu ya jirani baada ya yeye kuuza simu zao kufuatia marumbano.

"Mwezi wa kumi mwaka jana, nilikuwa namkataza kwenda kuomba simu. Alikuwa anaenda kwa jirani anaomba simu," Wafula alisimulia.

Aliongeza, "Nilikuwa na simu nikauza pamoja na yake. Niliziuza kwa sababu zilikuwa zinaleta shida kwa nyumba, hatukuwa tunaelewana. Kila mara alikuwa anashinda kwa simu. Alikuwa anapigia watu ambao sielewi wanazungumza sana. Nikimuuliza anakuwa mkali. Alikuwa anauliza  kwani sitaki azungumze na watu wa kwao. Lakini nikichunguza hakuwa anaongea na watu wa kwao. Alikuwa akipata simu anaenda FB na kuongea na watu wake.. Niliona niziuze tukae bila simu sisi wote wawili."

Wafula alidai kuwa baada ya kuuza simu zao, hali nyumbani iliimarika hadi wakati mpenziwe alipojuana na jirani ambaye alikuwa anamsaidia na simu yake.

"Tulikaa kwa muda wa takriban mwezi moja na amani wakati hatukuwa na simu. Sasa alipojuana na jirani alikuwa anaenda kuomba simu  na kupigia watu. Siku moja aliweza kutumiwa nauli akaenda na huyo jirani kwa soko. Nilimuuliza akaniambia kesho yake anaenda," Wafula alisema.

Aliendelea, "Huwa tunaongea na yeye lakini hatuelewani vizuri. Vile alienda nilipata nguvu ya kununua simu ingine na yeye akaenda akanunua simu ingine. Nimeshindwa kuoa. Ni kama alienda na roho yangu. Kama atarudi, wacha arudi na simu yake kwa sababu ako nayo, sitauza tena."

Bi Phanice hata hivyo alipingana na madai ya mpenziwe na kudai kwamba alikuwa na mipango ya kando, jambo ambalo lilisambaratisha mahusiano yao.

"Ni mambo na wasichana. Alikuwa anahanyahanya. Sitaki stori zake, nishamove on," Phanice alisema.

Aliongeza, "Mimi saa hii sitaki mahusiano, nataka kuwa single. Mimi sitaki kuwa na bwana saa hii. Nataka nifocus na mambo ya shule ndiyo nijue hatua itakayofuata. Wacha kwanza nifikirie."

Wafula alijaribu kujitetea kwa kusema, "Hadi nimekupeleka kwa Radio Jambo juu nakupenda. Nimekupeleka kwa radio kwa sababu nakupenda."

Bi Phanice alisema, "Mimi nilitoka huko nikarudi kwa mamangu. Nikasema nirudi shule kwanza. Saa hii nasoma sitaki mambo na mapenzi."

Wafula alipomuuliza ikiwa mpenziwe atarudiana naye baada ya kumaliza masomo, Bi Phanice alisema ,"Sina jibu hapo, nitafikiria."

Je, maoni yako ni yepi kuhusu Patanisho ya leo?