Kwenye Patanisho asubuhi ya Ahamisi kwenye stesheni ya Radio Jambo kipindi Gidi na Ghost Asubuhi, kijana Robert mwenye umri wa miaka 37 alitaka kupatanishwa na mkewe aliyesema alitoroka nyumbani mwezi jana.
Robert alisema mkewe walikosana na yeye baada ya kukorofishana kwa hulka ya kurudi nyumbani nyakati za usiku.
Robert alilaumu hatua ya mkewe kuondoka nyumbani kwa mpango wake wa kando ambaye alikuwa anachumbiana naye miaka 3 kabla ya mkewe kuja Nairobi.
Hata hivyo, alisema kwamba baada ya mkewe kuja kuishi naye miaka 3 iliyopita, alikatisha uhusiano huo lakini mkewe alikuja kuambiwa na alipoona mwanamke huyo akimpigia simu, alipandwa na mori na kuigura ndoa.
“Bibi yangu alikuwa ameenda nyumbani Desemba na watoto, tunakaa na yeye Kitengela, wakati anarudi, yeye hufanya kazi za mjengo. Nikampeleka mahali nilikuwa nafanya kazi kufanya na yeye, nikapigiwa simu na mama tuliyekuwa katika mapenzi kitambo kabla familia yangu ije Nairobi…”
“…baada ya familia kuja Nairobi nilivunja mahusiano, na mke wangu alipoona hiyo simu akaanza visirani, anarudi nyumbani usiku. Na sasa hivi yuko kwao Nakuru, na tangu aende tulikuwa tunazungumza na ananirushia mambo mbaya mbaya… aliacha watoto,” Robert alisema.
Wazazi wa mkewe walimtaka Robert atafute mahari kwanza kabla ya kuanza kudai mke, kwa vile wameshakosana, yeye kumfuatilia mkewe kwa wazazi ni kama kumchokoza mzazi.
Kwa upande wake, mkewe alipopigiwa simu, mara ya kwanza alikataa kuchukua simu lakini mara ya pili akachukua na kusema kwamba Robert amemsumbua sana na kwa muda mrefu.
“Ako na mipango ya kando wengi Nairobi, na pia alikuwa ananichapa sana. Nikiwa Nyumbani tayari alikuwa na wao. Sio watu wa ploti waliniambia, mimi niligundua mwenyewe. Mimi nimeamua kukaa peke yangu. Watoto ni wake nilimuachia. Wa kwanza ako na miaka 13, wa pili ako na miaka 9 na wa mwisho ni 5,” Mkewe alisema.
“Huyo jamaa alinipiga sana akaninyonga, hata watu wa ploti wanajua, niliamua niondoke tu juu angeniua,” aliongeza.
Robert alipopewa nafasi ya kuzungumza na mkewe, alimtaka kurudi nyumbani kulea watoto lakini mkewe alimgombanisha kwa lugha yao.