Katika Kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, kitengo cha Patanisho, kijana kwa jina Morris Evans Awiti kutoka kaunti ya Homabay alitaka kupatanishwa na mkewe Pauline Anyango.
Morris alisema kwamba wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 4 na watoto wawili lakini walikosana Ijumaa iliyopita kutokana na kile alichokitaja kama ni ‘mambo na mipango ya kando’.
“Aliona mdada mwingine alinipigia simu, huyo alikuwa rafiki yangu tukiwa shuleni. Sasa mke wangu akadhani ni mpango wangu wa kando. Sasa alinipigia kelele halafu nikamchapa na kiboko. Halafu akatoka na kuenda kwa nyanya yake,” Morris alisema.
“Meseji zangu, mke wangu aliona kwa Facebook nikimwambia huyo rafiki yangu kwamba nitakupigia baadae, sasa hivi niko busy. Mke wangu nilimpigia hata leo akasema amenisamehe lakini sijaamini ndio maana nimeleta patanisho,” aliongeza.
Anyango alipopigiwa simu, alipatikana amezima simu.
Morris alisisitiza kwamba licha ya mkewe kumuambia kuwa amemsamehe na anahitaji muda, yeye alikuwa anataka mtoto arudi ili aende shule.