Patanisho:Chelsea wakifungwa anakuwa mkali, analala kwa kiti, hakuli- Mke amlalamikia mumewe

Joy alisema hali imebadilika sana nyumbani katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

Muhtasari

•Joy alisema shida ulianza baada ya kuzozana kuhusu simu yake wakati mumewe alipomuomba ili atazame mpira.

•Bw Paul alipopigiwa simu hakuwa na mengi ya kusema ila alibainisha kwamba hana shida yoyote na mkewe.

Image: RADIO JAMBO

.Mwanadada aliyejitambulisha kama Joy Mulanda (23) kutoka Kasarani alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Paul Shimokoti (28) ambaye alikosana naye hivi majuzi.

Joy alisema ndoa yake ya miaka miwili imekuwa na misukasuko ila mambo yaliharibika zaidi siku mbili zilizopita wakati walikosana hadi mumewe akaanza kulala kwa kiti.

Alisema shida ulianza baada ya kuzozana kuhusu simu yake wakati mumewe alipomuomba ili atazame mpira.

"Siku ya Jumamosi, mume wangu aliniitisha simu ili atazame mechi ya Chelsea kwa sababu simu yake imeharibika. Jumapili akaniitisha tena atazame ya Man U. Nikamwambia ameniitisha sana, akakasirika," Joy alisimulia.

Aliongeza, "Alienda akalala kwa kiti, sasa haongei,  hakuli. Kila wakati Chelsea wakipigwa anakuwanga hivyo. Hata wakifungwa huwa anakuwa mkali, anakuwa kama radi. Huwa anakasirika mpaka mtoto akilia anasema nitakupiga wewe . Mara nyingi huwa anakasirika siku za mpira."

Joy alisema hali imebadilika sana nyumbani katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

"Ukimuongelesha ananung'una tu. Hajakula, anasema vitu zinatembea kwa tumbo. Marafiki zake huniambia akiwa na stress huwa anakuwa hivyo," alisema.

Pia alilalamika kuhusu tabia ya mumewe kuvaa mavazi yasiyo ya kuvutia licha ya juhudi zake kumshinikiza  avae mavazi mazuri.

"Mara nyingi nikimuomba pesa huwa na majibu makali. Nikimuuliza pesa ya salon anauliza kama nataka kutengeneza nywele ama kulipa nyumba. Nikimuomba pesa ya out anasema nataka out ama nataka kuishi. Huwa anavaa nguo hivyo hivyo hata unaogopa kutembea naye. Hawezi kuvaa luku. Sisi ni wadogo," alisema.

Bw Paul alipopigiwa simu hakuwa na mengi ya kusema ila alibainisha kwamba hana shida yoyote na mkewe.

"Hakuna shida inaendelea. Nampenda. Ata yeye anajua nampenda. Ni ile tu kisirani mingi ako na mingi. Hiyo ndiyo iko mingi," alisema.

Aliongeza, "Na madrama drama tu kila corner. Ndiyo maana mimi hunyamaza tu. Sitaki maneno mingi kwa hivyo njia ya maana ni kunyamaza."

Kuhusu malalamishi ambayo yaliibuliwa na mkewe, alisema, "Hizo ni mambo madogo tutaweza kushughulikia."

Je, ushauri wako ni upi?