Shoga Jude Magambo azungumzia uhusiano wake, afichua sababu ya kuanza kuchumbiana na wanaume

Jude Magambo almaarufu Manzi wa Meru ameweka wazi kuwa kwa sasa yuko kwenye mahusiano ya kimapenzi.

Muhtasari

•Alizungumza Jumatano katika kipindi cha Bustani la Massawe ambapo alikiri anachumbiana na mwanamume mwenzake, Rayton Sun.

•Alifichua kuwa mpenzi wake ndiye aliyemwendea kwa ajili ya kumtongoza.

ndani ya studio za Radio Jambo
Jude Magambo ndani ya studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO STUDIO

Mwanatiktok shoga, Jude Magambo almaarufu Manzi wa Meru ameweka wazi kuwa kwa sasa yuko kwenye mahusiano ya kimapenzi.

Mtayarishaji huyo wa maudhui mwenye utata alizungumza na mtangazaji Massawe Japanni siku ya Jumatano wakati wa kipindi cha Bustani la Massawe kwenye Radio Jambo ambapo alikiri kwamba anachumbiana na mwanamume mwenzake, Rayton Sun.

Alisema walikutana kwenye mitandao ya kijamii, wakazungumza na kufahamiana kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.

“Wakati huo nilikuwa na meseji nyingi, watu walikuwa wananitafuta ili kuchumbiana. Sijawahi kutamani kuchumbiana, Nairobi unachumbiana na watu wanachumbiana na wengine.

Sikuwa nimefikiria kuchumbiana. Ata sijui ilifika wapi mahali nikakubali ombi la kuchumbiana naye. Lakini tuko katika mahusiano mazuri,” Jude Magambo alisema

Alifichua kuwa mpenzi wake ndiye aliyemwendea kwa ajili ya kumtongoza..

"Wananikujia, mimi huwa simwendei mtu yeyote. Siwaendei watu,” alisema.

Alisema kuwa kwa sasa amechumbiana kwa miaka miwili, akifichua kuwa alivunjwa moyo hapo awali na kumfanya aogope kuingia kwenye mahusiano.

Jude pia alifichua kuwa kabla ya kuanza kuchumbiana na wanaume, katika siku za nyuma alikuwa akichumbiana na wasichana.

“Nimechumbiana na wanawake. Ilikuwa sawa lakini haikuwa nzuri kwangu. Sikupenda kwa sababu nilikuwa nipo, lakini sipo kwa wakati mmoja. Kwa sababu ninajinyima. Lakini kwa bahati yoyote nipate hisia kwa wasichana zimeanza kukua, nitaenda huko, "alisema.

Katika mahojiano hayo, Jude alikanusha kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu Brian Chira.

Mwanatiktok huyo shoga aliweka wazi kuwa yeye na Chira walikuwa marafiki wakubwa tu.

Alisema licha ya kuwa marehemu alionekana kutangamana naye kimapenzi hasa walipokuwa kwenye sehemu za burudani, hawakuwahi kufikia hatua ya kuchumbiana.

“Hapana, sikuchumbiana naye. Ingawa, alikuwa mguso sana haswa wakati amelewa. Lakini hatukuwahi kuwa na mazungumzo hayo ya kuchumbiana,” Jude Magambo alisema.

Aliongeza, "Alikuwa anastarehe nami, na mwenye kugusana sana. Singemwambia aache, ningemruhusu kwa sababu nilijua ni pombe na wakati fulani ataacha. Lakini hatufiki hatua hiyo ya kuchumbiana.”

Mwanatiktok huyp hata hivyo alibainisha kwamba watu wengi wanaamini kwamba walikuwa wakichumbiana, na kudai kwamba wengine sasa hata wanamwita mjane.

"Kwangu mimi sikuchumbiana na Chira," alisema.

Magambo pia alikiri kumkosa sana marehemu Chira.

Alifichua kuwa marehemu tiktoker huyo alipokuwa hai, walifanya mambo mengi pamoja na kutengeneza kumbukumbu zisizofutika zinazomsumbua hadi sasa.

“Nimem’miss sana Chira. Na nilikuwa nikishiriki naye mambo mengi. Wakati fulani, alikuwa kama ndugu yangu. Wakati ambapo naskia ako mbali, nilikuwa naskia kuna kitu kisicho sawa.

Haikuwa inaisha hadi wiki moja kama sijamuaona, ama siku tatu,” alisimulia.