Patanisho: "Nilioleka bahati mbaya, nilidanganywa nikapata jamaa amenioa"- Msichana wa miaka 18 akiri

"Nilioleka bahati mbaya. Nilidanganywa nikapata huyo jamaa amenioa. Ile shida napitia ni kubwa sana," Mercyline alisema.

Muhtasari

•Mercyline alisema uhusiano na mzazi huyo wake uliharibika baada ya kutoroka nyumbani na kuoleka akiwa na umri wa miaka 16 tu.

•Bi Mary alipopigiwa simu alisikika kufurahia sana kumsikia bintiye na alikubali ombi lake la msamaha mara moja.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mwanadada ambaye alijitambulisha kama Mercyline Wafula ,18, kutoka kaunti ya Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mamake mzazi Mary Lusike ,55,  ambaye alikosana naye takriban miaka miwili iliyopita.

Mercyline alisema uhusiano na mzazi huyo wake uliharibika baada ya kutoroka nyumbani na kuoleka akiwa na umri wa miaka 16 tu.

Alisema mamake alikasirika sana kwani alitoroka hata kabla ya kumaliza shule.

"Kwa sasa niko Baringo. Nilioleka bahati mbaya. Nilidanganywa nikapata huyo jamaa amenioa. Ile shida napitia ni kubwa sana," Mercyline alisimulia.

Aliongeza, "Saa hii mimi ni mjamzito. Nikipigia mzazi hashiki simu, nikipigia jamaa zangu hawashiki simu. Saa hii niko pekee yangu. Sina mtu wa kunisaidia kazi. Mzee akiamka anaenda kazi, sina mtu wa kunisaidia."

Alisema alimfahamisha mamake kuhusu hatua yake ya kuolewa baada ya kukaa mwaka moja kwenye ndoa

"Alisema ile uamuzi nilichukua, nipambane na hali yangu. Sasa najuta. Nilikuwa shule na nikatoroka hivyo hivyo tu," alisema.

Bi Mary alipopigiwa simu alisikika kufurahia sana kumsikia bintiye na alikubali ombi lake la msamaha mara moja.

"Nimekubali msamaha baba. Mtoto wangu alipotea anaitwa Mercy," Bi Mary alimwambia Gidi.

Mercyline alichukua fursa hiyo kunyenyekea kwa mzazi huyo wake na kuomba radhi kwa kutoroka nyumbani.

"Mimi ni mjamzito. Kama umenisamehe naomba nikuje nyumbani unishughulikie. Naweza kuja nyumbani muda wowote?" Mercyline alimwambia mamake.

Bi Mary alimjibu bintiye, "Asante sana. Nashukuru. Nimefurahi kuskia ni wewe. Mimi nimekusamehe. Nilikuwa nimekumiss muda wote. Kweli Mungu anasikia maombi yangu."

Alisema amefanya juhudi nyingi za kumtafuta bintiye katika kaunti ya Bungoma, Kakamega, hata Nairobi ila bado hajafanikiwa.

Kuhusu ujauzito wa bintiye, Bi Mary alisema, "Hiyo ni baraka ya Mwenyezi Mungu. Siwezi nikazuilia hiyo. Akikuja tutampokea kwa shangwe na nderemo."

Aliongeza, "Najiskia vizuri vile nimeongea na wewe. Mungu amlinde ndio akipanga safari nione ni yeye kweli."

Mercyline alisema, "Nataka niende nijifungue alafu nirudi shule. Mambo ya ndoa nitaangalia baadaye."

Je, una maoni ama ushauri upi kuhusu Patanisho ya leo?