Jamaa aliyejitambulisha kama Paul Gikundi ,27, kutoka kaunti ya Meru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake Moses Mutabari ,56, ambaye alikosana naye miaka mingi iliyopita baada ya kutofautiana nyumbani.
Paul alisema uhusiano wake na babake ulisambaratika akiwa katika shule ya msingi baada ya mzazi huyo wake kuzozana na mamake, jambo ambalo lilimpelekea kutoroka nyumbani mwaka wa 2007 akiwa na miaka 13.
"Kulingana na maongezi yake, ni kama sio baba yangu mzazi. Hata nikiwa shule ya msingi, alikuwa akigombana na mama yangu akimwambia anirudishe kwa baba yangu mzazi. Nilimuuliza shida ni nini akaniambia niambie mama anipeleke kwa baba yangu. Nikaona badala ya mama yangu akufe bure, nikajiondoa hapo," Paul alisema.
"Niliondoka nikiwa darasa la tano nikiwa na miaka 13. Nilimaliza shule ya msingi, nikatafuta kazi, na niko na familia sasa. Nikijaribu kuongea na yeye huwa ananitusi sana. Nilitaka niongee na yeye nione kama atakubali nirudi pale nyumbani. Mama yangu hatakangi kuniambia baba yangu ni nani. Naona ni kama aliaga dunia," alisema.
Bw Moses alipopigiwa simu, Paul alichukua fursa hiyo kuomba msamaha na kumsihi akubali arudi nyumbani.
"Naomba msamaha kama nilikukosea. Naomba kama unaweza kukubali nikuje nyumbani pamoja na familia tukae pamoja," Paul alimwambia babake.
Bw Moses alisikika kukubali ombi la msamaha la mwanawe ila akaweka wazi kwamba Paul sio mtoto wake halisi.
"Nimekubali msamaha, anaweza kurudi nyumbani. Sijawahi kumbagua, yeye mwenyewe ndiye alitoroka nyumbani. Nilioa mama akiwa naye, sasa huyo ni wangu?" Bw Moses alisema.
Aliongeza, "Sijawahi kumfukuza kwangu, lakini sijawahi kumfukuza. Yeye alitoka kwangu kitambo. Ni miaka mingi imepita."
Paul alisikika kufarijika baada ya babake kumsamehe na akasema kuwa atafanya mipango ya kurudi nyumbani.
Je, una maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?