Mwanadada aliyejitambulisha kama Brenda Akoth ,19, kutoka kaunti ya Kisumu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Phanuel Owino ,23, ambaye alikosana naye takriban wiki moja iliyopita.
Brenda alisema ndoa yake ya mwaka moja ilisambaratika wiki iliyopita wakati alipoondoka baada ya mumewe kumshtumu kwa kumdharau.
"Kila mara anasema namdharau. Eti akiniambia kitu sifanyi. Eti nakataa kupatia mtoto uji. Nilimkasirisha, akachoka na mimi, akaanza kuongea na wasichana wake wa kitambo. Kila mara yuko kwa simu, nilikasirika pia nikachukua vitu zangu nikapeleka kwa jirani. Saai niko kwa dada yangu. Jamaa hajulikani kwetu. Nilikuwa nahangaika ikabidi niingie kwa ndoa," Brenda alisema.
Aliongeza, "Mahali nilikuwa nimepeleka nguo walimdanganya eti mama ndiye aliniambia nitoke kwa hiyo boma. Kilichonikasirisha ni yeye kuchat na wasichana wake wa kitambo."
Phanuel alipopigiwa simu alikiri kwamba alianza kuzungumza na wasichana wengine ila akaeleza kwamba kuna sababu.
Alimshtumu mzazi mwenzake kwa kudhalilisha boma lao na kuweka wazi kwamba hayuko tayari kurudiana naye.
"Wewe umechukua boma letu kama takataka. Nilikwambia nimekupatia muda, kama ni kuoleka vile ulikuwa unataka kuoleka kwanza uoleke alafu ukipima uone ni wapi kulikuwa kuzuri ni sawa," Phanuel alisema.
Aliendelea, "Tangu nizaliwe sijawahi kuona mwanamke anakuja anapiga meza akiongea na mama mkwe.Kwa nyumba yangu hafai kupiga, lakini yeye anapiga meza kwa mama mkwe. Alafu anachukua mguu anaweka kwa ingine, anakaa vile anataka. Na anaongea akipayuka kwa nyumba ya mama mkwe. Tangu tuoane amekuwa mtu wa vituko. Alianza kunisumbua na wiki mbili. Nilijaribu kuvumilia lakini imefika mahali punda imechoka."
Brenda alijitetea akisema, "Mimi huwa siinui miguu naweka kwa meza ya mama mkwe. Nilikuwa na hasira nikipiga meza. Vile alikuwa anaenda juu, pia roho yangu inapanda. Baba mkwe alikuja lakini hakuniambia twende tutengeneze maneno."
Phanuel alisema, "Siko tayari kumkaribisha kwa sababu anatoka anarudi anaomba msamaha na akirudi anasema anataka kuenda kufanya kazi, anataka kuoleka. Kwa kijiji mzima alisema anatesekea hapo. Yeye aende ajaribu kwanza kama ni kuoleka alafu aweke kwa kilo aone ni wapi ni kuzuri. Kama ni hiyo kazi alitaka kufanya aende afanye kwanza. Hapo nimenawa mikono. Kwa sasa nataka nikae pekee yangu. Maneno ya wanawake sitaki. Yeye aende tu atulie, ajaribu mbinu. Mimi ni mwanaume. Wakati ataona arudi, atanipata. Nimejaribu kuangalia maslahi ya huyo mtoto. Nilimwambia niko tayari kushughulikia mtoto."
Brenda hata hivyo alibainisha kwamba tayari alikuwa amepata funzo lake na alikuwa tayari kurudi kwa ndoa yake.
"Hizo siku mbili nimeona vile dada yangu anaishi, imenifunza. Kila mtu ananiambia hakuna ndoa nzuri, lazima tu nivumilie," alisema.
Je, una ushauri ama maoni yapi kuhusu Patanisho ya leo?