Patanisho: Jamaa ajuta baada ya pombe kuvunja ndoa ya miaka 7, atoa ushauri maalum kwa walevi

"Pombe inaharibu boma, inaharibu kazi, inaharibu kila kitu..," Charles alishauri.

Muhtasari

•Charles alisema ndoa yake ya miaka 7 ilivunjika mwaka wa 2021 baada ya kuzozana na mkewe kuhusu tabia yake ya ulevi na vurugu kwa nyumba.

•Bi Fridah alipopigiwa simu alishika na kuelezewa kuhusu nia ya hatua hiyo ila akakata simu yake muda mfupi baadaye.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Charles Chomba ,40,  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake  Fridah Gakii ,29, ambaye alikosana naye takriban miaka mitatu iliyopita.

Charles alisema ndoa yake ya miaka saba ilivunjika mwaka wa 2021 baada ya kuzozana na mke wake kuhusu tabia yake ya ulevi na vurugu kwa nyumba.

"Mimi nilikunywa pombe mpaka tukakosana. Ilifika mahali akawa ananitusi na tunapigana. Nilikuwa najaribu kuacha pombe nashindwa. Baada ya yeye kuenda niliweza kuacha. Niko na kama miezi sita tangu kuacha pombe.  Niliona sio vizuri kuwa nakunywa kama iliniharibia ndoa. Wakati huo pesa haikuwa inakaa kwa mfuko. Sasa hivi naweza kukaa na pesa kwa mfuko bila kunywa pombe," Charles alisimulia.

Aliongeza, "Wakati mwingine huwa anasema anaweza kurudi. Wakati mwingine anasema hawezi. Nilienda kwao mama mkwe akasema hiyo ni mambo yetu tunafaa kutatua sisi wawili. Tuko na watoto watatu pamoja. Nilichukua watoto wawili kwa sababu nilikuwa nahisi upweke sana. Niko nao hapa nyumbani. Huwa namwambia niliacha pombe, lakini haamini. Nikimwambia anaona kama ni mchezo."

Charles aliomba kusaidia kujua msimamo wa mkewe kuhusu wao kufufua ndoa yao.

Bi Fridah alipopigiwa simu alishika na kuelezewa kuhusu nia ya hatua hiyo ila akakata simu yake muda mfupi baadaye.

Charles alisema, "Labda yuko kazi. Nimefuatilia lakini ako tu nyumbani. Mamake anasema tuongee kivyetu turudiane. Nimeenda na mjomba mara kama mbili. Nikaenda mpaka na wamama wengine hapo, lakini shida ni yeye. Anasema atarudi akitaka. Na muda unaenda. Nitajaribu kuongea na yeye ataniambia vile anataka. Ningependa kumwambia msamaha ni wa maana bora mtu abadilike tuweze kulea watoto."

Pia alikuwa na ushauri maalum kwa watumizi wa pombe.

"Pombe inaharibu boma, inaharibu kazi, inaharibu kila kitu..," alisema.

Je, una maoni ama ushauri upi kuhusu Patanisho ya leo?