Watangazaji Gidi na Ghost wamsherehekea gwiji Leonard Mbotela akitimiza miaka 84 (+video)

Walimsherehekea Bw Mbotela kama mtu wanayemwiga na kupongeza kazi yake nzuri na maisha marefu ambayo amekuwa nayo.

Muhtasari

•Ghost alibainisha kuwa mtangazaji huyo mkongwe ni rafiki yao mkubwa na pia ni shabiki wa kipindi chao cha asubuhi kwenye Radio Jambo.

•Pia walimtakia maisha marefu na yenye afya mtangazaji huyo mkongwe.

na Gidi katika picha ya maktaba.
Mwanahabari mkongwe Leonard Mambo Mbotela na Gidi katika picha ya maktaba.
Image: GIDI OGIDI

Siku ya Jumatano asubuhi, watangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi na Jacob Ghost Mulee walimsherehekea mtangazaji mkongwe wa redio na TV Leonard Mambo Mbotela ambaye anasherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Watangazaji hao wawili mahiri walimsherehekea Mbotela kama mtu wanayemwiga na kupongeza kazi  yake nzuri na maisha marefu ambayo amekuwa nayo.

“Leo ni siku ya kuzaliwa kwa gwiji wa utangazaji hapa nchini Kenya Leonard Mambo Mbotela ambaye anatusikiza sasa hivi. Huyu ni jamaa ambaye ameishi miaka 84,” Gidi alisema moja kwa moja hewani wakati wa kipindi cha asubuhi Jumatano.

Kwa upande wake, Jacob Mulee alibainisha kuwa mtangazaji huyo mkongwe ni rafiki yao mkubwa na pia ni shabiki wa kipindi chao cha asubuhi kwenye Radio Jambo.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars slibainisha kuwa wamejifunza mengi kutoka kwa Bw Mbotela ambayo yamewasaidia kuwa watangazaji wa kusherehekewa pia.

“Hiyo ni baraka ya Mwenyezi Mungu Gidi. Na ni rafiki yetu kwa dhati, nisikilizaji pia wa Radio Jambo. Na sisi utangazaji wetu tumetoa kwa Gidi kama yeye. Kwa hiyo, Kheri ya siku ya kuzaliwa Maje Maje,” Ghost alisema.

Watangazaji hao wawili waliendelea kufanya mzaha kuhusu kipindi maarufu cha  ‘Je, huu ni Ungwana’ ambacho Bw Mbotela alijulikana nacho kabla ya kumuimbia wimbo wa ‘Happy Birthday’. Pia walimtakia maisha marefu na yenye afya mtangazaji huyo mkongwe.

Takriban mwaka mmoja uliopita, Gidi na Ghost walikutana na mkongwe Leonard Mbotela na kushiriki naye mazungumzo ya wazi.

Gidi alishiriki baadhi ya nyakati nzuri walizokuwa nazo na gwiji huyo wa utangazaji kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Katika mkutano huo, Mambo Mbotela alifichua kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Radio Jambo na vipindi vyake vizuri.

“Mimi nakiliza sana Radio Jambo. Nakiliza zaidi zaidi, baadhi ya mazungumzo yenu na ucheshi wenu. Lakini kuna kipindi ambacho chaitwa Patanisho, mimi huwa sisiki kabisa. Ikifika saa mbili na nusu, niko na nyinyi. Ile mkianza tu, niko na nyinyi,” Mambo Mbotela aliwaambia Gidi na Ghost.

Aliongeza, “Kuna zingine huwa zinanichekesha sana, zingine zinanishangaza, zingine zinamchekesha hata Ghost.

Mtangazaji huyo wa zamani wa runinga ya KBC alibainisha kuwa Radio Jambo ni mojawapo ya vituo vya redio vinazopendwa na kusikilizwa sana nchini Kenya.

“Muendelee hivyo hivyo, sisi twaipenda na kutumai kwamba kutakuwa na vipindi vingine vizuri vizuri vitakuja,” alisema.

Mambo Mbotela pia aliwapongeza watangazaji Gidi na Ghost kwa kazi yao nzuri na kuwashukuru kwa kuwajengea asubuhi mamilioni ya Wakenya ambao hufuatilia kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi.