Patanisho: Jamaa apigwa kalamu kwenye uwanja wa ndege kwa kutumia bangi, miraa

"Nilikuwa natumia bangi, miraa na ile ya wahindi. Nilidhani wasiponiona hawawezi kujua," Rabo alisema.

Muhtasari

•Rabo alisema uhusiano wake na rubani huyo wa ndege uliharibika Agosti mwaka jana baada ya yeye kufutwa kazi kwa kutumia mihadarati.

•Bw Waweru alipopigiwa simu, Rabo alichukua fursa hiyo kumuomba msamana na kumsihi warejeshe uhusiano mzuri.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Jamaa ambaye alijitambulisha kama Silvester Rabo ,28, kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na rafiki yake Captain Waweru.

Rabo alisema uhusiano wake na rubani huyo wa ndege uliharibika Agosti mwaka jana baada ya yeye kufutwa kazi kwa kutumia mihadarati.

"Kuna mahali nilikuwa nimeandikwa kazi alafu nikafukuzwa . Walisema hawatanipa mkataba mwingine. Nilikuwa naongea na Kapteni Waweru, akauliza nini ilifanya nifukuzwe. Nikamwambia nilichoambiwa. Baadaye akapatana na mtu mwingine akamwambia nilikuwa natumia mihadarati. Kuna wakati tulipatana na Kapteni akaniambia anajua nilifukuzwa juu ya mihadarati, yeye alichukua kama mimi ni muongo," Rabo alisimulia.

Aliongeza, "Singependa kukosana na huyo kapteni Waweru. Nilikuja kujua nilifukuzwa kwa sababu ya mihadarati. Nilikuwa natumia bangi, miraa na ile ya wahindi. Nilidhani wasiponiona hawawezi kujua. Ningetaka tuelewane na yeye kwa sababu ata haniongeleshi. Niliachana na mihadarati. Saa hii niko sober kwa mwaka moja unusu."

Bw Waweru alipopigiwa simu, Rabo alichukua fursa hiyo kumuomba msamana na kumsihi warejeshe uhusiano mzuri.

"Nathamini urafiki wetu na sitaki tuharibu uhusiano. Mimi nakuomba msamaha, kama utaweza naomba unisamehe," alisema Rabo.

Bw Waweru alikubali kumsamehe Rabo na kumwambia, "Usijali kaka yangu. Acha nikutafute. Sisi ni binadamu. Huwa tunafanya makosa. Bora unajifunza nayo, ndio muhimu."

Pia aliahidi kumtafuta kijana huyo na kuzungumza naye baadaye.

Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?