Patanisho: "Moyo wangu ni mgonjwa sana!" Mke aumizwa na maneno makali ya mumewe na mama mkwe

"Mbona hutaki kunisikiliza nikikwambia kitu? Niliskia vibaya. Moyo wangu ni mgonjwa sana," Jentrix alilalamika.

Muhtasari

•Jafred alisema ndoa yake ya miaka 6 iliingia doa siku ya Jumatatu wakati mkewe alipokosana na mamake na kutoroka.

•Jentrix alipopigiwa simu alilalamika kuhusu mama mkwe kutawala ndoa yao na mumewe kupendelea kumsikiliza mama.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Jafred Mulwa ,27, kutoka Mumias alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Jentrix Nyongesa ,27, ambaye alikosana naye hivi majuzi tu.

Jafred alisema ndoa yake ya miaka 6 iliingia doa siku ya Jumatatu wakati mke wake alipokosana na mamake na kutoroka.

Alisema mkewe alizozana na mama yake kabla ya kuchukua hatua ya kuenda kwao.

"Mke wangu alikuwa anatengeneza boma. Vile mama alikuwa anatoka kulima akakuja kumshauri jinsi ya kutengeneza. Mke wangu akaskia vizuri akaanza kutusiana na mama yangu. Mama akaenda kwa rafiki yangu akanipigia simu akanieleza kilichotokea," Jafred alisimulia.

Aliendelea, "Mke wangu pia alinipigia simu kisha akatoroka akaenda kwao. Baadaye nilipigia mamake simu nikamuuliza kwa nini akikosana na mamangu anaenda kwao. Pia yeye nilimuuliza mbona akikosana na mama anakimbia kwao. Hapo sasa tukaanza kugombana. Ilifanyika jana, lakini sio mara ya kwanza. Tulitusiana vibaya nikamwambia kama hataki kukaa pamoja na mama yangu aseme."

Jentrix alipopigiwa simu alilalamika kuhusu mama mkwe kutawala ndoa yao na mumewe kupendelea kumsikiliza mama.

"Mama yake alinipata kama natengeneza mlango ya nyumba, akaniambia huwa hawatengenezi hivyo. Nikamwambia aache nijaribu. Akaanza maneno alafu akaenda akaambia kijana.Kijana badala asikilize sisi wote, anasikiliza mama yake. Mimi sikumtusi. Mume wangu aliniambia nitoke hapo nimwachie watoto. Muulize kati ya mama yake na yeye nani anafaa kunicontrol?," Jentrix alilalamika.

Jafred alimlalamikia mkewe kwa kuchukua hatua ya kutoroka kila anapokosana na mama mkwe.

"Nakuomba unapokosana na mama, usikimbie kwenda kwenu," alimwambia mkewe.

Jentrix alimwambia, "Mbona hutaki kunisikiliza nikikwambia kitu? Niliskia vibaya. Moyo wangu ni mgonjwa sana. Mimi sikutaka maneno mingi, mimi nilitoka kuhepa maneno."

Jafred alimalizia kwa kumwambia mkewe jinsi anavyompenda.

"Mimi nakupenda sana kama mke wangu. Wewe kaa na mama, mkikosana uniambie. Ninapokukosea nipigie simu, nakupenda," alisema.

Jentrix alisema, "Bado nina machungu juu ya mambo mama yake na yeye aliniambia."

Je, ushauri ama maoni yako ni yepi kuhusu Patanisho ya leo?