Patanisho: "Nilimuuliza shida ni nini, akaanza kulia!" Mama mkwe azungumzia sababu ya bintiye kugura ndoa

"Nilimwambia aniambie ni nini kilifanyika akatoroka, akaanza kulia," Bi Jesca alisema.

Muhtasari

•Inganga alidai kwamba mkewe alitoroka, kisha akaja kugundua baadaye kuwa mama mkwe ndiye alisababisha ndoa yake kuvunjika.

•Jesca alipopigiwa, alibainisha kwamba hata yeye hajui mahali binti yake yupo huku akitupilia mbali madai ya kuvuruga ndoa yake.

Ghost na Gidi studioni
Image: RADIO JAMBO

Joseph Inganga ,24, kutoka Siaya alituma ujumbe akitaka kupatanishwa na mama mkwe wake Jesca Ouma kwa madai kwamba alivuruga ndoa yake.

Inganga alidai kwamba mkewe alitoroka, kisha akaja kugundua baadaye kuwa mama mkwe ndiye alisababisha ndoa yake kuvunjika.

"Tulikosana mwezi wa nne akaenda kwao. Kumbe mama mkwe ndo alikuwa anaharibu ndoa. Mke wangu alienda kwao, nikaenda kuzungumza na wazazi wake, mamake akasema nisimchukue kwanza, eti nikae siku tatu ndo niende nimchukue.

Nilikaa siku tatu nikaenda, mamake akaanza kuniambia eti ametoroka hajui mahali ako, kumbe alikuwa anajua mahali ako," Inganga alisema.

Alisema kwamba angependa mama mkwe amueleze ikiwa mke wake atarudi ama la.

"Mke wangu alirejesha watoto kisha akaenda mahali anaishi. Niko nao kwa boma.Mke ananiambia atarudi," alisema.

Bi Jesca alipopigiwa, alibainisha kwamba hata yeye hajui mahali binti yake yupo huku akitupilia mbali madai ya kuvuruga ndoa yake.

"Kurudi anaweza kurudi lakini vile alienda ata simu alizima, sijui mahali ako.Wacha nimtafute, nikimpata nitamwambia akuje. Nikimpata nitamrejesha nyumbani tuongee. Natamani arudi kwa watoto lakini simpati. Alifunga simu yake. Nikimpata lazima atarudi kwa watoto," Bi Jesca alimwambia Inganga.

Aliongeza, "Kulipa mahari sio lazima. Kitu kizuri ni mtoto kuoelewa. Alikuja nyumbani, nikimuuliza shida ni nini analia tu.  Mara ya mwisho aliniambia anarejesha tu watoto alafu arudi nyumbani. Nikamwambia asiache watoto wateseka. Nilimwambia aniambie ni nini kilifanyika, akaanza kulia. Vile alifika, Joseph aliniambia mke wangu aliacha watoto akaenda."

Joseph alidai kwamba alizozana na mkewe baada ya mzazi huyo mwenzake kuchukua namba za simu ambazo alikuwa ameenda kwa karatasi.

"Nilitoka kazini, hakuwa anaongea. Akasema kuna kitu nilichukua. Ilikuwa tu manamba kwa karatasi, zilikuwa namba za wanaume. Niliona nimnyang'anye simu, akanipiga ngumi. Nami nikampiga makofi mawili," alisema

Je, una maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?