Patanisho: Mwanadada atemwa baada ya kupost mabishano yake na jamaa kwenye Facebook

"Kuna kitu ulipost iliudhi watu wa nyumbani. Mimi sina shida kwako lakini vitu ulipost zilileta shida," Martin alimwambia mkewe.

Muhtasari

•Cecilia alisema ndoa yake ya takriban mwaka 1 ilisambaratika wiki jana baada ya kusumbuana na mumewe kwa muda.

•Cecilia alikiri kwamba alipost screenshot ya mabishano yake na jamaa kutoka nyumbani kwa akina mumewe.

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Cecilia Nzisa Mutua ,31, kutoka Kibwezi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Martin Sabaya Meeli.

Cecilia alisema ndoa yake ya takriban mwaka 1 ilisambaratika wiki jana baada ya kusumbuana na mumewe kwa muda.

Alisema mara kwa mara mumewe amekuwa akimpiga, kumtusi na kumuonyesha madharua huku akimsamehe.

"Tumekuwa tukikosana mara kwa mara.. Huwa namsamehe lakini anarudia kunipiga. Huwa ananishuku kuwa na wanaume akienda kazi. Nimejaribu hadi kumpa line zangu aende nazo kazini. Lakini kila saa huwa ananishuku niko na wanaume. Sasa ananitumia tu meseji za matusi kwa simu. Nilimwambia nilimpenda, na kabla ya kumpenda nilifanya kazi na wanaume, lakini sikuwapenda," Cecilia alisimulia.

Aliongeza, "Tuliachana na baba ya watoto wangu watatu. Hatukuwa tumeoana, ilikuwa tu urafiki, sikuwa nimeamua kuolewa wakati huo. Mimi ndio nashughulikia watoto wangu. Mimi ni mjamzito, anajua. Na amenikataza kufanya kazi, na hanisaidii ilhali nina watoto nyumbani."

Bw Martin alipopigiwa simu, Cecilia alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha huku akimweleza anavyoteseka.

"Mimi nakuomba msamaha juu nateseka. Tumbo inaniuma, watoto wanasumbua," Cecilia alisema.

Martin alimuomba mkewe ampigie simu wazungumze huku akieleza kwamba kuna kitu alipost ambacho kiliibua shida.

"Kuna kitu ulipost iliudhi watu wa nyumbani. Mimi sina shida kwako lakini vitu ulipost zilileta shida,' alimwambia mkewe.

Cecilia alikiri kwamba alipost screenshot ya mabishano yake na jamaa kutoka nyumbani kwa akina mumewe.

"Nilikuwa nimepost kwa Facebook. Ni jamaa alinikosea kwa simu akiongelea watoto wangu. Nikamuuliza ni nini anaingilia watoto wangu. Ni jamaa wa kwao. Nilishafuta kitambo," alisema.

Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?