logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Patanisho: Jamaa apata meseji za kutisha kwenye simu ya mkewe, azozana na jamaa aliyemsindikiza mkewe

Jacob alisema ndoa yake ya miaka 12 ilivunjika mwezi Novemba 2021 baada ya mkewe kupata kazi ya hoteli na kuanza madharau.

image
na Samuel Maina

Vipindi22 August 2024 - 06:11

Muhtasari


  • •Jacob alisema ndoa yake ya miaka 12 ilivunjika mwezi Novemba 2021 baada ya mkewe kupata kazi ya hoteli na kuanza madharau.
  • •Stella alipopigiwa simu alisikika kuwa na machungu na mzazi mwenzake na alikuwa mfupi wa maneno.

Mwanaume aliyejitambulisha kama Jacob Ogari Nyandieka ,39, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Stella Cherono ,36, ambaye alitengana naye takriban miaka mitatu iliyopita.

Jacob alisema ndoa yake ya miaka 12 ilivunjika mwezi Novemba 2021 baada ya mkewe kupata kazi ya hoteli na kuanza madharau.

"Aliondoka Novemba 2021. Tulikuwa tumekaa tu vizuri kabla apate kibarua. Baada ya kupata kibarua ya hoteli akaanza kuja amechelewa.

Wakati mmoja alinidanganya eti bosi wake amemwambia afanye kazi saa 24. Nilimwambia hiyo haiwezekani. Baadaye nilipata akitayarisha watoto akaenda. Nikasema kama ameamua kuenda ni sawa badala ya kubishana naye," Jacob alisema.

Jacob alisimulia jinsi mkewe alianza tabia za kushukiwa hadi hatimaye akaamua kuchukua watoto wao wawili na kuenda.

"Siku moja niliona amezidikishwa na jamaa. Huyo jamaa akaanza kunitishia akiuliza kama huyo ni bibi yangu. Ilikuwa karibu tupigane, watu wa ploti wakatuzuia. Walimwambia huyo jamaa kwamba Stella ni mke wangu na tuko na watoto.

Baadaye alianza kuchelewa zaidi, kulala nje na kutorudi nyumbani. Kazi alikuwa anafunga kabla ya saa kumi na moja. Nilimuuliza mwajiri wake akasema wafanyikazi wake wanafanya kazi hadi saa kumi na moja, sio masaa 24.

Pia nilikuwa napata meseji kwa simu yake. Katika meseji moja, niliona jamaa anamuuliza kwani aliamua mtoto wake. Nikamuuliza ni mtoto yupi huyo aliua. Nikawa sielewi kabisa mambo yake," alisema.

Jacob alisema kwamba licha ya kutengana, amekuwa akiwasiliana na mzazi huyo mwenzake pamoja na watoto wao.

"Huwa tunaongea hata na watoto. Hivi majuzi aliniambia anataka kurudi," alisema.

Stella alipopigiwa simu alisikika kuwa na machungu na mzazi mwenzake na alikuwa mfupi wa maneno.

"Mwambie kwanza kunitukana. Amekuwa akinitumia meseji za matusi," Stella alisema kabla ya kukata simu.

Baada ya Stella kukata simu, Jacob aliendelea kufunguka mengi zaidi kuhusu masaibu ya ndoa yake.

"Wakati alienda, nilikuwa nampigia simu anapatia jamaa mwingine ananitusi. Ndio maana nilikasirika...Watoto wananiambia wanataka kutoka ushago. Mama yake alisema ataniambia siku nitaenda. Nimengoja hadi nimechoka," alisema.

Aliongeza, "Nataka kujua msimamo wake. Nikimuuliza kama ameolewa anasema hajaolewa. Sitaki kuanza familia nyingine, napenda familia yangu.Ni uchungu.'

Jaribio la kumpata Stella tena ili kueleza msimamo wake halikufua dafu kwani hakushika simu wakati Gidi alimpigia.

Katika ujumbe wake wa mwisho kwa mzazi mwenzake, Jacob alisema, "Stella nakuomba tafadhali, uko na chance katika maisha yangu. Rudi tulinde watoto wako. Rudi nyumbani, kila kitu changu ni chako. Licha ya yote uliyonifanyia, mimi nakupenda. Usiache watoto wetu wahangaike."

Je, una maoni ama ushauri upi kuhusu Patanisho ya leo?


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved