Patanisho: Baba akataa kushika simu za bintiye baada ya kuacha shule kwenda kuolewa

"Mtoto kama huyo naweza kufikisha hata kortini akiendelea kufanya mambo ambayo hayaeleweki," Bw George alitishia.

Muhtasari

•Beryl alisema uhusiano wake na babake uliharibika mwaka wa 2022 wakati mzazi huyo wake alimshinikiza atoke kwa ndoa yake aende kuishi naye ila hakutaka.

"Huyo ni mtoto wangu lakini wana mambo mengine hayaeleweki. Sina shida. Mambo mengine tunaweza kuzungumza," Bw George alisema.

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Beryl Adhiambo ,24, kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake mzazi George Odhiambo ,45, ambaye alikosana naye takriban miaka miwili iliyopita.

Beryl alisema uhusiano wake na babake uliharibika mwaka wa 2022 wakati mzazi huyo wake alimshinikiza atoke kwa ndoa yake aende kuishi naye ila hakutaka.

"Shida ilianza wakati niliacha shule nikiwa kidato cha 3. Nilishika mimba ikabidi niende niolewe kwa huyo jamaa. Baba alitaka niende kwake Mombasa. Alituma fare niende kwake lakini sikuenda. Nilijifungua kitambo. Bado niko na bwana, huwa hatuonngeleshani na baba. Nilijaribu kumpigia baba simu hakushika," Beryl alieleza.

Aliongeza, "Mama aliaga dunia nikiwa na miaka 10. Tulilelewa na nyanya baada ya baba na mama kukosana 2006. Baba ata hakumzika mama."

Bw George alipopigiwa simu, Beryl alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha na kumuomba awe akipokea simu zake.

"Mbona nikikupigia hupokei simu zangu. Naomba kama nilikukosea unisamehe," Beryl alimwambia babake.

Bw George alisema, "Wewe mbona unakaa hivyo??.. Huyo ni mtoto wangu lakini wana mambo mengine hayaeleweki. Sina shida. Mambo mengine tunaweza kuzungumza. Nimekuwa nikizungumza naye miaka hii yote."

"Mimi sina shida na yeye. Hizo tabia zake za kuchukua hatua ambazo hazieleweki, angeuliza. Kwa nini nikose kushika simu zake kama hasikilizi maneno. Ukiona baba amekwambia hataki hii, unaacha tu," aliongeza.

Beryl aliendelea kulalamikia kuhusu mzazi huyo wake kutopokea simu zake na akamuomba waweze kurejesha uhusiano mzuri.

"Huwa nampigia simu hashiki. Mimi sijui chenye anataka. Nilikuwa nataka tu ashike simu nikimpigia. Ningependa tuongee vile tulikuwa tunaongea kitambo," alisema.

Bw George alisema, "Mtoto kama huyo naweza kufikisha hata kortini akiendelea kufanya mambo ambayo hayaeleweki."