Jamaa aachwa baada ya mkewe kurudi ghafla na kumpata na mwanamke mwingine saa tano usiku

Violet alisema mumewe alikuwa na mahusiano na mwanamke mwingine, na alimtesa sana katika miaka 3 ya ndoa yao.

Muhtasari

•Davis alisema ndoa yake ya miaka 4 ilisambaratika Agosti mwaka jana wakati mkewe alipompata na mwanamke mwingine.

•"Saa hii nimekonda juu ya stress, watu wanashinda wakiniangalia kwa barabara. Roho yangu yote iko kwako," Davis alisema.

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Davis Opakwa (30) kutoka kaunti ya Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Violet Anyanzwa (26) ambaye alikosana naye mwaka jana.

Davis alisema ndoa yake ya miaka 4 ilisambaratika Agosti mwaka jana wakati mkewe alipompata na mwanamke mwingine.

Alidai kwamba Bi Violet aliondoka na kumuachia mtoto wao wa miaka miwili.

"Alienda mwaka jana mwezi wa nane, huwa anakuja kutembea. Mimi ndiye niko na mtoto. Tunaongea tu vizuri lakini wakati mwingine unaskia amekasirika. Mwanzoni alikuwa anasema babake anasema niende kwao ili arudi. Baadaye babangu alienda wakazungumza na babake. Babake pia alinipigia akaniambia msichana ndiye anakataa kurudi," Davis alisimulia.

Alidai kwamba amekuwa akifanya mipango ya kuenda nyumbani kwa kina mkewe ila bado hajapata fedha za kutosha.

"Alimuacha mtoto akiwa na miaka miwili. Tangu amuache, mimi ndiye nimekuwa nikimshughulikia. Nikienda kazini huwa nampeleka day care. Akienda kwao huwa anakuja anamchukua baadaye anamrudisha. Wakati mwingine huwa anakuja anakaa siku mbili alafu anaenda. Nimeshindwa kumuelewa," alisema.

"Nimefanya uchunguzi wangu nikaona kitu inafanya tunakosana, ni ile akitoka kwangu huwa ananiambia ameenda kwa ndugu yake. Lakini nikichunguza nimegundua kuna mwanaume alikuwa na yeye. Nikimuuliza ananiambia ni mjomba wake. Sasa hivi anasema ako kwa kakake. Nililelewa na mama wa kambo na maisha ilikuwa ngumu, singependa mtoto wangu apitie maisha kama  hayo," aliongeza.

Violet alipopigiwa simu, aliweka wazi kwamba hataki kurudiana na mzazi huyo mwenzake na akamtaka atafute mke mwingine.

Aidha, alifichua kwamba Davis alikuwa na mahusiano na mwanamke mwingine, na alimtesa sana katika miaka 3 ya ndoa yao.

"Mwambie aendelee na maisha yake. Nilimove on. Nimekaa naye miaka mitatu, hiyo miaka tatu ameoa mwanamke mwingine, yeye kwa nyumba moja na mimi nyingine. Alikuwa ananifanyia madharau navumilia tu juu ya mtoto.Mimi huyo siwezi," Violet alisema.

"Nilienda nyumbani matanga ya nyanya yangu. Akawa hanisaidii nikiwa nyumbani. Kutoka nyumbani kurudi kwangu, nikampata na mwanamke. Kumuuliza akasema hakuna cha kuongelea, akaniacha kwa nyumba  akaenda na mtoto bila hata kuacha kitu ya kula. Mimi nikaona nimevumilia sana nikaenda. Nikaenda nyumbani alafu nikaja Nairobi kufanya kazi. Nilikuwa naenda kutembea ili kuona mtoto, yeye anafikiri bado tuko pamoja. Nikamuuliza anataka nimsamehe wakati ata hajaenda kwetu. Anasema nikae hapo anitafutie pesa ya kuenda nyumbani," aliongeza.

Huku akijitetea, Davis alisema mwanamke ambaye mkewe alishuku kwamba alikuwa na mahusiano naye alikuwa jirani yake kutoka nyumbani ambaye alikuwa ameenda Nairobi kwa ajili ya kazi.

"Huyo mwanadada ni wa huko nyumnbani kwetu. Alikuwa amekuja kazi, alafu mwenye alikuwa anawasiliana na yeye simu ilizima. Mimi nikamwambia akuje alale kwa kitu kwa sababu mama mtoto anakuja. Mama watoto alikuwa amezima simu, ata hakuwa ameniambia anakuja. Nilijaribu kumwambia nikapata amezima simu," alisema.

Violet hata hivyo alikanusha maelezo ya mumewe na kuweka wazi kwamba hakuwahi kuzima simu yake.

"Aki wewe ni muongo. Sijawahi kuona muongo kama wewe.Vile ulienda na mtoto, si ulijua utalea?Ndio mtu aamue kutoka kwake, sio rahisi. Tangu nitoke kwake niko na amani kabisa. Nataka tu hiyo amani peke yake. Nimevumilia sana na huyo mwanaume," Violet alisema.

Davis alisema, "Mimi sina amani. Tangu aende naamka saa kumi na moja kutayarisha mtoto kabla niende kazini. Mimi bado nakupenda. Hakuna mwanamke mwingine."

Violet akajibu, "Hiyo ni uongo. Mimi siwezi kuamini. Ata kama babangu huwa simuamini, wewe ndiye nitaamini... Aishi vizuri, atafute mwanamke mwingine. Aache stress mingi atakufa mapema."

"Saa hii nimekonda juu ya stress, watu wanashinda wakiniangalia kwa barabara. Roho yangu yote iko kwako," Davis alimalizia kwa kusema.

Je, maoni ama ushauri wako ni upi?