Kijana aliyejitambulisha kama Henry Kahaba ,20, kutoka Teso Kaskazini alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mjomba wake Evans Ekada ,40, ambaye alikosana naye miaka miwili iliyopita.
Henry alisema uhusiano wake na mjomba wake uliharibika Januari 2022 wakati alipotoroka kwake baada ya kuzozana naye.
Alisema chanzo kuu cha mzozo wake na mjomba wake ilikuwa ni shangazi yake ambaye alimchochea mjomba.
"Nilikuwa naishi kwa nyanyangu. Mamangu aliniacha huko nikiwa mdogo. Nilikuwa nalelewa na mjomba wangu na nyanyangu. Shangazi yangu alikuwa ananichukia sana. Mjomba wangu alikuwa anamskiliza sana. Mjomba alikuwa akinilalamikia kwamba nagombana na shangazi yangu. Hiyo ilifanya mjomba wangu akanichukia sana. Ilifika wakati tukagombana hadi tukapigana. Alinipiga nikaona hapo sitoboi nikaamua kutoka kuja Nairobi," Henry alisimulia.
Baada ya kuenda Nairobi, alianza juhudi za kumtafuta baba yake, ingawa hakufaulu.
"Nilimuuliza mamangu anionyeshe familia yangu. Mamangu akawa ananizungusha akiniambia atanionyesha familia yangu. Mtu mwingine aliniambia babangu alikufa. Sasa hivi niko Nairobi nafanya kazi. Babu yangu alikuwa ananipenda sana. Nadhani shangazi yangu ndiye alifanya nisipewe shamba," Henry alisema.
Bw Evans alipopigiwa simu, Henry alichukua fursa hiyo kuomba msamaha.
"Naomba msamaha kwa yale yalitendeka kati yangu na wewe. Nilikukosea sana. Naomba unisamehe," alisema.
Bw Evans alimwambia, "Mimi sina shida yoyote na wewe. Hiyo iliisha. Si wewe ndiye ulitoka ukaenda?"
"Alikuwa kijana kijana mdogo wakati huo. Akuje Krismasi tumchinjie jogoo. Asikuwe na wasiwasi. Sidhani ako na shida kubwa na mke wangu," Bw Evans aliongeza.
Wawili hao waliweza kupata na wakakubaliana kurejesha uhusiano mzuri kati yao.
Je, una maoni au ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?