Nicholas Mukasa ,33, kutoka Umoja alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Catherine Ochieng' ,32, ambaye alikosana naye hivi majuzi.
Nicholas alisema ndoa yake ya miaka sita ilisambaratika wiki moja iliyopita wakati mkewe alitoroka kufuatia mzozo wa kinyumbani.
Alisema uraibu wake wa pombe ulipelekea yeye kumkewe kutoroka kwani ulikuwa unamfanya ampige.
"Kwa miaka sita iliyopita, shida imekuwa pombe. Wakati mwingine nikikunywa nakuwa mkali, hiyo ndo imeharibu mambo. Juzi tulizozana nikamchapa, akakasirika. Nilitoka kurudi nikapata ameenda. Anakaa na rafiki yake, sijui ni wapi ako. Aliacha kila kitu akaenda na mtoto," Nicholas alisema.
Aliongeza, "Tumekuwa tukiongea lakini stori ya kurudi ndo hataki, anasema nimpatie muda. Nimejiangazia na nikaamua kuacha pombe. Nilitumia pombe mara ya mwisho wiki moja iliyopita wakati alienda."
Catherine alipopigiwa simu, alifichua kwamba mumewe amekuwa na mazoea ya kumpiga hata wakati hajalewa.
"Sio juzi pekee yake. Huyo mtu ana vurugu sana, amezoea. Huwa ananipiga hata wakati mwingine kama hajalewa. Vurugu ilianza hata kabla nizae. Amejaribu kuongeleshwa na watu haskii," Catherine alisema.
"Muulize ni mara ngapi amenishikia kisu? Hata niko na picha ingekuwa ni WhatsApp ningewatumia. Imekuwa ni vita kubwa sana. Yeye bora ametoka, hataki kujua mambo iko aje kwa nyumba. Alafu kila mara anakushtumu na mtu yeyote, ata huwezi kuongea na mtu," aliongeza.
Huku akijitetea, Nicholas alisema, "Wakati ukikunywa, unahisi tu kuwa na vurugu. Nilimuomba msamaha nikamwambia nimeachana na pombe. Huwa hatupigani kila wakati, ni wakati unaenda kwa baa na masaibu ya hapa na pale yanakuzidia. Cate mimi naomba msamaha kwa mambo ambayo imetokea. Naomba uweke yote nyuma na tuendelee vizuri."
Cate alimwambia, "Nimepitia mengi sana kwa mikono yake. Anipee muda nipone. Ingekuwa ni mara moja, ingeeleweka. Lakini vile amezoea, anipee muda nipone. Baadaye nitajua."
"Awe na muda ajue ni nini anataka. Wakati wowote akiambiwa atokee, ata hataki kujua kama kuna kitu kwa nyumba, anatokea anaenda kulewa.Nimetoka mara kadhaa. Anakuja tunaongea. Baada ya siku mbili, tunarudi palepale. Mtu anakuja kwa nyumba anapika, Akikula akishiba, vita inaanza," Cate aliongeza.
Nicholas hata hivyo alidai kwamba amebailika na kumuahidi mkewe kwamba ataacha vurugu.
Cate alisema, "Ni ngumu kujua kama amebadilika ama ni huduma zangu amemiss kwa nyumba. Kwanza abadilike. Hata hajui barabara kama kuna nyasi ama lami.."
Huku akieleza sababu ya kutowahi kwenda kwa kina mkewe, Nicholas alisema, ".Aliniambia nitapigwa. Aliniambia watu wa kwao wako preserved."
Cate alimwambia, "Yeye ajibebe tu aende."
Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?