Kijana aliyejitambulisha kama Victor Ouma ,24, kutoka Gem alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake Nahashon Otieno ,51, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.
Victor alisema uhusiano wake na babake uliharibika Agosti 2024 kufuatia mzozo wa kinyumbani.
Alidai kwamba babake alimkana, akauza vitu vyake na kubomoa sehemu ya nyumba yake.
"Nilikosana na baba yangu 2024. Mi hukaa Nairobi, nikaenda kutengenezewa driving license. Nilipata baba yangu ameuza vitu zangu , kondoo. Nilienda kuuliza kwa nini baba sijaona mbuzi mahali nilikuwa nimezifunga. Ndugu yake akaanza kunigombanisha. Kumbe baba aliuza, akachukua pesa akaenda kulewa na ndugu zake. Niliambia nyanya kwamba baba amezoea, mwanzoni aliuza ng'ombe. Nilisema lazima nitoe saut," Victor alisimulia.
Aliongeza, "Baada ya hapo walianza kutupa maneno wakisema hapo sio kwetu niende nitafute mama. Tayari baba alikuwa amekosana na mama na akaondoka. Keshoye asubuhi aliniambia hataki kuiniona hapo niende nitafute mama, akasema yeye sio baba yangu. Nilienda kutulia kwa rafiki yangu. Baba alianza kubomoa nyumba yangu. Walibomoa nusu, nikaenda kwa chifu."
Victor alilalamika kwamba licha ya kumfukuza, babake na ndugu zake bado wamekuwa wakimsumbua kwa kumpigia simu.
"Mama ndiye mwenye kusema anajua baba yangu. Kama mtu amekufanyia hivyo, pesa namtumia, anauza vitu zako, na haoni mambo umemfanyia. Hiyo si ni madharau. Imeniuma sana," alisema.
"Baba ndiye alinionyesha mahali ya kujenga. Nilijenga 2019. Nilienda Nairobi, nilikuwa naenda nyumbani baada ya wiki moja, Alikosana na mama, akaanza kuniingilia. Wakati mama alikuwa, hangechukua vitu na kuuza ovyo ovyo," aliongeza.
Victor alisema kwamba ni baada ya kwenda kupiga ripoti kwa polisi ambapo mama yake alimfichulia kuwa Bw Nahashon sio baba yake mzazi.
"Niliambia mama, akasema alikuja na mimi nikiwa mdogo. Wakati walitaka kuoana, baba alikuwa anasema aache mtoto huko alikuwa. Nilikuja kujua hayo juzijuzi wakati tulienda kwa kituo cha polisi. Wakati uko na pesa wanakupenda sana, wakati huna pesa wanakugeuka sana," alisema.
"Nilitaka asinisumbue na simu, wananisumbua sana,"
Juhudi za kumpata Baba Victor hata hivyo hazikufua dafu.
Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?