Brian Omondi ,28, kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Esther Vulemi ambaye alikosana naye mwaka uliopita.
Brian alisema ndoa yake ya mwaka mmoja ilisambaratika Agosti mwaka jaba wakati mkewe alipoondoka na kwenda bila sababu.
"Nilikosana na mke wangu 2023. Nikiangalia mahali nilimkosea sikuona. Nilipitia mambo mengi na huyo msichana. Nimejaribu njia zote nikashindwa nikaona leo nije Patanisho," Brian alisema.
Aliongeza, "Tulikuwa naye nyumbani, nikaenda kazi ya pikipiki. Kurudi nilipata nyumba haina kitu, haina mtu. Nilikuwa naleta breakfast nikapata hakuna mtu. Nilikuwa nashughulikia mahitaji yote. Nikimpigia simu tunaongea kidogo alafu anakata. Dada yake ndiye ameharibu bibi yangu. Yey ndiye alimtumia nauli atoke Nairobi."
Baada ya kushinikizwa kusema ukweli, Brian alikiri kuwahi kuwa na mpango wa kando.
"Mpango wa kando haiwezi kosa. Nilikuwa nimesema nimeacha," alisema.
Esther alipopigiwa simu alifunguka kuhusu jinsi mumewe alikuwa akimpiga.
"Wakati wenye tulikuwa naye hatukuwa
sawa. Kunipiga kila siku. Nilikuwa na ball, akanipiga nikiwa na ball mpaka
mtoto akaja kutoka. Kunipiga nayo alikuwa ananipiga, mpaka kwa makosa ambayo haiko.
Anafanya boda, alikuwa na wanawake wengi. Nikimuuliza ananipiga," Esther alisema.
Brian alijitetea kwa kusema, "Katika mila yetu, ukiwa na mimba, uanze kutembea na wanaume wengi huko nje, mpaka huyo mtoto akufe ama awe na shida. Ilikuwa tu kutokana na hasira, nikampiga kidogo. Nilimpata red-handed akiwa na mtu. Mimi naomba msamehe, "
Esther alisistiza kwamba shida kuu ya mumewe ilikuwa ni kumpiga.
"Anataka turudiane ndiyo animalize kabisa. Aliambia dadangu wasipokuja kunichukua watanichukua nikiwa maiti. Mimi sioni," alisema.
Brian aliomba msamaha na kudai kwamba amebadilisha tabia zake.
"Ninaapa mbele ya dunia nilibadilika. Ata yeye anajua. Nimepitia mengi na huyo msichana ndiyo maana sitaki tuachane. Pia yeye alikuwa anahanya. Sijafichua uchi wake kabisa kwa sababu bado nampenda... Nimeomba msamaha, ilikuwa ni hasira. Nilibadilika, nimechange aki. Nataka turudi pamoja. Kumbuka yote ambayo tumepitia na wewe. Ata wewe ni mengi umenikosea, lakini huwa nakumbuka magumu ambayo tumepitia. Ata kama utanipea muda, ni sawa," alisema.
Esther alisema, "Mimi nimekusamehea lakini siamini katika mara ya pili. Sioni tukienda mahali. Kupitia magumu sio suala. Na hukunipiga mara moja, umenipiga mara mingi hata ukikatazwa. Nimezoea kuishi pekee yangu. Sina ubaya na wewe. Nilitaka tu ujue ukweli kunihusu. Kama ni salamu, hiyo ni sawa."
Brian hakuwa na budi ila kukubali uamuzi wa mpenziwe.
Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?