Tony Baraza ,34, kutoka Webuye alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Purity , 28, ambaye hajakuwa katika maelewano mazuri naye.
Tony alisema ndoa yake ya miaka mitatu iko matatani baada ya yeye na mkewe kukosana mwezi uliopita.
"Tunakaa pamoja lakini maelewano sio mazuri. Nikitoka kazi napata tu amenuna kwa nyumba. Haongei. Nikienda kazi ndio ananitumia meseji za makasiriko tu. Ananiandikia mambo kama, unaona mimi sio mwanamke, unaona mimi ni mjinga. Nyumba haikaliki," Tony alisema.
Aliweka wazi kwamba hajui sababu ya mkewe kumkasirikia huku akitupilia mbali kukosa uaminifu ama kutoshughulikia mahitaji ya nyumbani.
"Siongei na mwanamke mwingine. Mahitaji na nyumbani nashughulikia yote," alisema.
Purity alipopigiwa simu, alifichua kwamba hakupendezwa na tabia ya mumewe kuongea na wanawake wengine akitoka kazini.
"Shida yake ni kuenda kazi alafu jioni anakuja tu kushinda kwa simu na kuongea na wasichana. Niliona namba kwa simu nikimuuliza inakuwa ni makosa. Sio mara moja, ni kama mara mbili. Nilimwambia shida ni hizo manamba tu. Nilimpata akiongea nao, nikimuuliza anaanza kunikasirikia. Hizo namba nilifuta naye akakasirika. Mmoja anaitwa Joyce, mwingine ni Grace. Labda kuna wengine, sijui," Purity alisema.
Huku akijitetea, "Hao tunafanya nao kazi. Ata yeye amewahi kuja nikamuonyesha. Huwa tunaongea tu mambo ya kazi."
"Niliachana na kazi ya kina Grace, niko na kazi yangu. Tuishi vizuri tuongeleshane juu hiyo kazi niliacha. Wewe unacheka na watu alafu nikikuja unanyamaza. Mimi nakaa na uoga tu. Mimi sikujua hiyo ndiyo shida. Naomba unisamehe tukae na amani," aliongeza.
"Ni sawa nimekusamehea, hakuna shida ingine. Nilikuwa nimekukasirikia, pole kwa hiyo pia. Sitamkosea hivyo tena," Purity alijibu.
Katika maneno yake ya mwisho, Tony alimwambia mkewe, "Nakupenda sana na sitaki tukosane tena. Hakuna kitu napenda hii dunia kama wewe."
Kwa upande wake, Purity alisema, "Mume wangu mi nakupenda. SIkuwa na maneno mengine ni hayo tu. Nakupenda kama mume wangu... Leo nauliza saa kumi na moja itafika lini, atapata nimemchemshia maji."