Pastor John Beth ,34, kutoka Kiambu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Beth ,30, kutoka Uganda ambaye aliondoka nyumbani mwaka jana na hajarudi.
John alisema mke wake alienda nyumbani mwezi Oktoba baada ya mwaka mmoja wa ndoa yao kwa ajili ya kuona watoto lakini hajawahi kurudi.
"Mwezi wa kumi tulikubaliana aende aone watoto wake Uganda. Nilipomuoa alikuwa amekaa sana bila kuona watoto wake. Nilimpata akiwa na watoto watatu tukachumbiana kwa miezi kumi. Nikamshughulikia akaenda," John alisema.
Aliongeza, "Hadi wa leo hajaweza kurudi. Bado sikuwa nimeenda kuona wazazi wake. Huwa namtumia pesa arudi na hakuji."
Gidi aliweza kuzungumza na mamake Beth ambaye alibainisha kwamba bintiye aliondoka nyumbani mwaka jana akidai kwamba anarudi kwa ndoa yake.
"Alienda. Sijamuona tangu wakati huo. Sijamuona mpaka sai. Bibi yake aliniambia wacha arudi huko. Tangu wakati huo sijawahi kumuona. Watoto wako kwa baba yao. Mimi niko na mmoja yule mdogo," mamake Beth alisema.
John alisikitika kusikia kwamba mkewe aliondoka nyumbani na hajawahi kufika kwake.
Mamake Beth alisema bintiye alikuwa amekosana sana na baba watoto wake kwa hiyo sio rahisi kwamba alirudi kwake.
Patanisho hiyo iligonga mwamba kwani haikujulikana aliko Beth.