Raphael Mureithi (27) kutoka Maua alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Nadia Ndevi (24) ambaye alikosana naye mwaka jana.
Raphael alisema uhusiano wake na Nadia wa miaka mitatu uliharibika Aprili mwaka jana kuhusiana na masuala ya kikazi.
Pia alikiri kuwa muongo sana kwa mkewe, jambo ambalo lilichochea wao kukosana.
"Tulikosana na mke wangu. Nilikuwa naendesha malori. Tukaanza kuwa hatuskizani. Akiniambia nikuje nakataa, mpaka akaona kama mimi ni muongo. Nakubali nilikuwa muongo, lakini nataka nimuombe msamaha juu nampenda," Raphael alisema.
"Hatusikizani, nataka nimuombe msamaha nione kama atanisamehe. Shida ilikuwa mambo ya kazi na uongo. Nilikuwa namdanganya juu ya kazi, sasa anaona kama niko na wengine. Wakati tulikosana, alikuwa na kazi yake Maua. Alitaka kuja Meru lakini hiyo siku bosi akanipigia akaniambia niende Machakos. Mimi kuenda Machakos nilidhani narudi, ikawa siwezi rudi hiyo siku. Kumwambia akakasirika, kutoka hapo hatuelewani," aliongeza.
Nadia alipopigiwa simu, Raphael alichukua nafasi hiyo kuomba msamaha na kuahidi kubadilika.
"Nilitaka nikuoimbe msamaha mbele ya Wakenya juu naona nilikukosea na uongo yangu. Nimekuwa muongo lakini nimeona nibadilike juu umekuwa wa maana sana kwangu," Raphael alimwambia mkewe.
Nadia alisema, "Bora tu urekebike. Amekuwa tu muongo, kukaa na mtu kama huyo na sio eti amekuoa ni ngumu. Akirekebisha uongo yake sina shida na yeye. Hakuna wanadada wengine.Niliona kukaa naye ni ngumu juu hawezi kuambia ako wapi, hawezi kuambia kitu atekeleze "
Raphael aliahidi kuacha kuwa muongo na hata akaeleza nia ya kuacha kazi ili kuangazia mahusiano yao.
"Uongo nimeamua kurekebika. Kama ni kazi ya magari nataka kuacha kazi tukae sasa. Nitatafuta mbinu. Naweza anza tu kazi ingine. Nadia nakuahiudi mbele ya Wakenya wote kwamba nitaacha uongo. Nitafanya mipango tuwe tunapatana ata kama ni mwezi mara moja, mimi wakati mwingine huwa silali, nafanya kazi hadi masaa 24. Kama kuna mtu hunipea matumani kwa maisha ni wewe. Bila wewe naskia sina matumaini. Siwezi kulinganisha na wanawake wengine," Raphael alisema.
Nadia alimwambia, "Nimemsamehe juu ameahidi atabadilika."
Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?