Jamaa aliyejitambulisha kama Enock Wafula (27) kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mercyline Khamala (24) ambaye alikosana naye mwaka wa 2023.
Enock alisema ndoa yake ya miaka minne ilisambaratika Septemba 2023 wakati alipozozana na mkewe kuhusu ushirikiano wake na shemejiye ambaye alidai alikuwa anampotosha.
Alisema mkewe alishikana na mke wa nduguye wakaanza kuenda nje ya ndoa, suala lililozua shida kwenye ndoa yake na ya nduguye.
"Wakati tulikuwa kwa ndoa na yeye, nikitoka kuenda kazi, nilikuwa naambiwa pia yeye anatoka. Kitu iliyotuharibia, yeye ni mtu wa kusikia maneno ya watu sana. Alishikana na bibi ya ndugu yangu, nikitoka pia wao wanatoka. Walikuwa wanaenda nje ya ndoa," Enock alisimulia.
"Ndugu yangu ilifika mahali akajua, kutoka hapo hawaelewani. Ndugu yangu alikasirika akaenda kikazi. Wakati nilimkataza mke wangu kutembea na watu ambao wanaharibu ndoa, alikataa kuskia akaenda kwao. Baadaye niliskia ako Embu kikazi. Tulizaa naye mtoto mmoja naye alikuwa na msichana alikuja naye. Sasa hivi watoto wako kwao. Huwa nashughulikia watoto vizuri. Ningependa nirudiane na mke wangu ili watoto wasihangaike," aliongeza.
Mercyline alipopigiwa simu, mwanzoni alisikika kukataa kabisa kurudiana na mzazi huyo mwenzake akibainisha kwamba alimkosea na hata akaoa mwanadada mwingine.
"Siwezi rudi. Mwambie iliisha hivyo juu . Mtu akuache kwa ploti na anaenda na mtoto wangu. Alishaoa, mimi sina haja na yeye, ashughulikie huyo mwenye ako nyumbani. Ata wakati tulikosana haikuwa vibaya sana. Aliskia mambo ya watu akafanya ndoa iharibike," Mercyline alisema.
"Tulikuwa tunaishi vizuri, maneno ya watu ndiyo ilifanya nitoke huko. Ni mtu mzuri, alikuwa anashughulikia msichana mwenye nilioleka na yeye. Hata wakati alishikwa, kama ningekuwa mtu mbaya, ningeenda na watoto wangu, nilivumilia tu," aliongeza.
Mwanzoni, Enock alisikika kupuuzilia madai ya kuwa na mke mwingine kabla ya kukubali kwamba alikuwa amechukua mwanadada mwingine ambaye aliachana naye mwaka jana.
"Ningependa turudiane. Mahali imefikia naona turudiane na tuache maneno mingi watoto wapate mwelekeo. Makosa yako naijua, na pia wewe unajua makosa yangu," Enock alimwambia mkewe.
Mercyline hata hivyo alisikika kuwa mgumu kubadilisha mawazo na akaibua madai ya kupigiwa na mpenzi wa mumewe ambaye alimuonya kuhusu uhusiano wao.
"Wewe mwenyewe ulinikasirikisha. Mtoto ako nyumbani, na anaingia shule, na hujatuma karo. Juzi huyo bibi yako sijui alitoa namba yangu wapi, alinipigia kuniambia maneno mbaya. Mimi sina shida na wewe, lakini kurudiana itakuwa kukudanganya," alisema.
Alipoulizwa kuhusu mazungumzo yake na mpenzi wa mumewe, Mercyline alisema, "Aliniambia kuniambia ati mimi nazungumza na mume wake. Anasema ati kuna mambo tunapanga na mume wake. Mimi sijawahi kumpigia simu."
Enock alisema ,"Nilikuwa na yeye (mke mwingine), ikabidi nimwambie apana. Wazazi walikataa. Huyo msichana alirudi kwao mwezi wa kumi. Huyo alienda kwao, niliachana na yeye "
Baada ya mazungumzo ya wazi, Mercyline alisikika kuyeyusha moyo wake na akakubali kurudiana na mumewe ila kwa masharti.
"Anajua mahali tulianzia na mahali tulifika. Tuling'ang'ana sana. Roho yangu bado ni ngumu. Ameona msichana ameenda kwao ndio ananitafuta mimi. Kama atabadilika mwenendo ni sawa tutapatana. Kama hatabadilisha hatutaweza," Mercyline alisema.
Katika maneno yake ya mwisho kwa mkewe, Enock alisema, "Merciline mimi ningependa turudiane na kusikuwe na shida. Mimi nakupenda wewe, nakumbuka mahali ulinitoa ndoa maana nimefikiria hayo."
Mercyline alisema, "Yeye ni bwana wangu, sijakataa. Ata kama tutarudiane lakini abadilike. Sijamkataa, nimekubali lakini abadilike."