Jamaa aliyejitambulisha kama Peter Alumasi ,48, kutoka kaunti ya Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake wa zamani Caroline Auma ,30, ambaye alikosana naye miaka mingi iliyopita.
Peter ambaye ana mtoto mmoja na Caroline alikiri kwamba ndoa yake ya mwaka mmoja ilivunjika kutokana na suala lake la kupenda wanawake sana.
"Mimi nilikuwa msherati, ilikuwa sababu ya kupenda wanawake sana ndio bibi akaenda," Peter alisema.
Alisema tangu mkewe aondoke hajaweza kutulia na mwanamke mwingine yeyote kwa ndoa.
"Wakati nilifungia mwanamke mlango, nikapata mwanamke mwingine huko Malava ndiiye akaniharibu akili. Sasa nimejaribu kuoa, wanaenda. Sasa nataka kuomba msamaha huyo bibi anisamehe, kama nilimkosea kwa sababu ya wanawake. Wakati nilienda town nikapata mwanamke mwingine aliniambia nitabeba roho ya wanawake. Mpaka leo sijaweza kuoa. Wanaenda kwa sababu ya usherati. Mimi ni msherati mkubwa sana, napenda wanawake," alisema.
Aliongeza, "Yeye akirudi, nitaomba msamaha. Mimi nimepata shida kubwa sana kwa sababu ya kupenda wanawake. Nikirudiana na yeye nitaacha usherati, nitaenda kwa kanisa."
Caroline alipopigiwa simu, Peter alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha na kuahidi kuacha usherati.
"Naomba msamaha kwa sababu ya kupenda wanawake. Ninaomba msamaha kwako unisamehe. Vile tumeachana, nimepata shida kubwa. Nitaacha mambo ya wanawake na nirudi kanisani. Naomba unisamehe. Najua kabisa napenda wanawake sana, naomba unisamehe.Sijapata baraka kwangu, kila mwanamke nikioa wanaenda," alimwambia Caroline.
Caroline kwa upande wake alithibitisha kwamba waliachana kitambo sana, mwaka wa 2001.
Ingawa aliweka wazi kwamba hajaolewa, alibainisha kwamba hawezi kurudiana na mzazi huyo mwenzake.
"Tuliachana kitambo. Tuliachana 2001. Sijui kwa nini ananitafuta. Mimi naishi tu maisha yangu. Hakuna nafasi ya kurudiana na yeye," Caroline alisema.
Peter alisema, "Nataka arudi nyumbani, natafuta kila mwanamke anaenda. Kijana wetu akuje ajenge boma nyumbani."
Juhudi za kuwapatanisha wawili hao hazikufua dafu kwani Caroline alishikilia msiammo wake kwamba hawezi kurudiana na Peter.