"Alikuwa ananipiga, anapiga mtoto wa miezi 10 kama mtu mzima" Mke alia akisimulia dhuluma katika ndoa

Kenneth pia alikiri kwamba alimpiga mkewe kutokana na hasira.

Muhtasari

•Kenneth alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika mwezi wa nne wakati mkewe alipotoroka.

•Jackline alifunguka kuwa uchungu kuhusu jinsi mzazi huyo mwenzake alikuwa anampiga pamoja na mtoto wake.

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Kenneth Simiyu Otaya ,26, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Jackline Naliaka ,24, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.

Kenneth alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika mwezi wa nne wakati mkewe alipotoroka.

Alidai kwamba mkewe alisikiliza sana maneno ya watu, jambo lilifanya atoroke.

"Tulikosana mwezi wa nne akaenda. Alikuwa anasikiliza maneno ya watu sana. Kuna watu wa ukoo hawakuwa anataka nikae na mke wangu. Ilitokea, mimi nilikuwa naishi na mama. Baba alikuja akauza shamba akamaliza, sikuwa najua. Wakati nilitahiriwa niliambiwa baba aliuza shamba akaenda Naivasha.

Wakati nilikua hadi nikaoa wakaja wakaambia bibi. Alikasirika kuskia sina chochote baba aliuza. Mpaka wazazi wake wamekuja wakanikasirikia. Saa hii nakaa na nyanya ambaye amezaa baba," Kenneth alisema.

Kenneth pia alikiri kwamba alimpiga mkewe kutokana na hasira.

"Nikimpigia huwa tunaongea lakini mambo ya kurudiana haniambii. Hiyo kusikiliza maneno ya watu nilikuja nikakasirika na nikamkwaruza kidogo. Nilimpiga," alisema.

Jackline alipopigiwa simu, alidai kwamba mumewe ndiye alikuwa anasikiliza maneno ya watu.

Aidha, alifunguka kuwa uchungu kuhusu jinsi mzazi huyo mwenzake alikuwa anampiga pamoja na mtoto wake.

"Alinipata nikiwa shule, kidato cha nne. Tukaanza mahusiano, akanipea mimba nikajifungua ata kabla nifanye mtihani. Hakutaka ata nifanye mtihani, lakini mama yangu akanisihi nifanye mtihani. Alikuwa anataka niende Kisumu ata nisifanye mtihani. Baada ya mtihani akaniruka.

Mimi nilienda kwa nyanya yake. Nikawa nampigia simu hakuwa anashika. Baadaye akaja nyumbani, kidogo kidogo akanipiga. Tulitoka nyumbani tukahamia Nyeri, alikuwa ananipiga bado, hadi anapiga mtoto wa miezi kumi kama mtu mzima. Alikuwa anasema sio mtoto wake, na ni mtoto wake. Nimekuwa kama mtoto mwenye hana baba, hata kusalimia mtu ananipiga. Maisha yangu imekuwa tu ya kupigwa, mimi nimechoka," Jackline alisema.

Kenneth alisema, "Kumpiga sikatai nilikuwa nampiga. Tuliongelea hiyo maneno ikaisha. Sikuwa napiga mtoto."

Jackline alisisitiza kwamba suala la kupigwa ndilo lilifanya akatoroka.

Mtangazaji Gidi alibainisha kwamba Patanisho haingeweza kuendelea kwa vile simu ya Jackline ilikuwa na tatizo. 

"Mambo ya vita katika mahusiano haifai. Nitaachia hiyo Patanisho hapo. Pole sana Bwana Simiyu, hii hatuwezi tukakusaidia," Gidi alisema.

Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?