Jamaa aambiwa mimba ya mkewe imemkataa baada ya kuwatembelea wakwe zake ili kumrudisha

Emmanuel alisema mkewe alimuachia mtoto wao mwingine wa miaka miwili.

Muhtasari

•Emmanuel alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitatu baada ya kutokea mzozo wa kinyumbani.

•Bw Ogolla alifichua kwamba Emmanuel alikuwa amefika nyumbani kwake na akamueleza jinsi ya kurejesha ndoa yake.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi, kitengo cha Patanisho, Emmanuel Okuku kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Elizabeth Katieno ambaye alitoroka wiki moja iliyopita.

Emmanuel alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitatu baada ya kutokea mzozo wa kinyumbani.

Alifichua kwamba Bi Elizabeth ambaye ana ujauzito wa mtoto wao wa pili alimuachia mtoto wao mwingine  wa miaka miwili.

"Mimi hufanya kazi Nairobi. Nikiwa huko huwa natuma shopping. Mwezi Januari nilikosa pesa. Nilimwambia avumulie akakataa kunielewa," alisema.

Emmanuel alisema alimfuata mkewe nyumbani kwao ila mashemeji wake wakaonekana kuweka vikwazo.

"Nikienda kwao naambiwa mimba imenikataa," alisema.

Kwa kuwa Bi Elizabeth hana simu, baba yake, Bw Ogolla alizungumza kwa niaba yake.

Bw Ogolla aliweka wazi kwamba mzozo wa bintiye na mumewe sio mkubwa kiasi cha kupatanishwa kwenye redio.

Bw Ogolla alifichua kwamba Emmanuel alikuwa amefika nyumbani kwake na akamueleza jinsi ya kurejesha ndoa yake.

"Nilizungumza na yeye na nikampatia mkakati wa kuongea naye. Nilimwambia tutazungumza tuone jinsi mke wake atarudi," alisema.

Huku akijitetea, Emmanuel alisema nyumbani kwa kina mkewe ni mbali sana na kwa sasa hayupo katika hali nzuri ya kifedha.

"Kwao na kwetu ni mbali sana. Alitakaa niende na wazee. Kwa sasa sina pesa" alisema.

Alidai kwamba aliagizwa kuenda na shilingi elfu kumi ambazo hana uwezo wa kupata kwa sasa.

Bw Ogolla hata hivyo aliweka wazi kwamba hajadai mahari yoyote kutoka kwa mkwe huyo wake ila angetaka kuketi chini naye pamoja na Elizabeth ili kuwapa ushauri wa ndoa.

"Huyu si msichana wa kwanza kupeleka kwenye ndoa. Huyu ni mtoto wangu wa pili kupeleka kwenye ndoa. Mimi sihitaji mahari. Ninachotaka, hao wawili kukaa kwa amani kwenye ndoa. Sitaki binti yangu kila wakati kurudi nyumbani na karatasi," alisema.

Aliongeza, "Nilitaka kijana wangu akuje nyumbani tuwafunze njia ya kukaa kwenye ndoa. Huyo kijana nilimwambia akuje tuzungumze naye akuje nimuonyeshe njia ya kuishi."

Gidi alimshauri Emmanuel kuchukua hatua ya kuenda kwa kina mkewe kama alivyoagizwa ili kurejesha ndoa yake.

Bw Ogolla alimtaka Emmanuel kuandamana na mzee mmoja hadi kwake siku ya Jumatano wiki ijayo, agizo ambalo alikubali.