"Kama si kutupatanisha nitakata simu!" Jamaa aliyeachwa kwa ulevi amtishia Gidi kwa hasira

"Yeye ni international kwa ulevi. Yeye alimaliza degree ya ulevi sasa imebaki tu Masters!" Diana alimlalamikia mumewe.

Muhtasari

•Sammy alisema alikosana na mkewe takriban wiki tatu zilizopita kufuatia tabia yake ya ulevi na kujihusisha na mipango ya kando.

•Huku akijitetea, Sammy alibainisha kwamba tayari ameacha ulevi na kumsihi mkewe akubali kurudi nyumbani.

•Wakati Diana alipojaribu kumuuliza hakikisho kuwa ameacha ulevi, Sammy alisikika kupandwa na mori na akadai kujua msimamo wake.

Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho siku ya Alhamisi, Sammy Juma (24) kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Diana Nafula (20) ambaye aliondoka ghafla na kumuacha  mwezi uliopita.

Sammy alisema alikosana na mkewe takriban wiki tatu zilizopita kufuatia tabia yake ya ulevi na kujihusisha na mipango ya kando.

"Nilienda nikakunywako kidogo alafu nikarudi nyumbani kama nimelewa. Bibi akaanza kisirani kidogo. Kwa hiyo harakati, sijui kama nilimpiga, hata sikumbuki. Asubuhi niliamka nikapata kama ameenda," Sammy alisimulia.

Aliongeza, "Nikijaribu kumtafuta kwa simu ameniweka blacklist. Ni kama alienda kwao. Sikufuatilia kwani niliogopa kupigwa. Nilikuwa nakaa nikingoja atarudi ndio nikaona nikuje Patanisho. Nisaidieni tu."

Diana alipopigiwa simu, mara moja alifunguka kuhusu tatizo la ulevi la mzazi huyo mwenzake na jinsi ambavyo hajakuwa akimpa motisha wa kutimiza ndoto yake ya kuwa mtangazaji.

"Si vibaya kupatanishwa lakini unaskianga mtu international kwa ulevi. Yeye alimaliza degree ya ulevi sasa imebaki tu Masters. Nilitaka niwe mtangazaji lakini mtuata hakupei motisha wa kufika mahali unataka, mtu kama huyo mnapelekana wapi?" alisema Diana.

Aliendelea, "Niliamua kumuondokea lakini sikumpea taarifa. Ilibidi kuondoka. Mtu akirudia kosa na unamwambia lakini hasikii!"

Huku akijitetea, Sammy alibainisha kwamba tayari ameacha ulevi na kumsihi mkewe akubali kurudi nyumbani.

"Hiyo mambo ya ulevi niliacha kitambo. Nimekaa sana nikikungoja. Hata ngombe ambaye nilkununulia amezaa juzi. Kuja unisaidie tafadhali. Niliacha ulevi," alisema.

Wakati Diana alipojaribu kumuuliza hakikisho kuwa ameacha ulevi, Sammy alisikika kupandwa na mori na akadai kujua msimamo wake.

"Mimi nataka uniambie kama hurudi nijipange.Usisikie mambo ya kina Gidi hawakujui. Wewe rudi nyumbani. Sitaki stori mingi," alisema.

Sammy ambaye alisikika kujawa na ghadhabu pia aliwageukia Gidi na Ghost na hadi kutishia kukata simu iwapo hangetetewa.

"Kama si kutupatanisha nikate simu. Mkiongea hivyo hatarudi. Mimi nimesema nilibadilika!" Sammy alisema kwa hasira.

Diana aliweka wazi kuwa hakupendezwa na jinsi mzazi huyo mwenzake alivyozungumza na kulalamika kuwa hata hakumpatia motisha wa kurudi.

Kufuatia hayo, aliweka wazi kuwa harudi na kumtaka Sammy asonge mbele na maisha yake.

Sammy hakupinga uamuzi wa mkewe kutorudi ila kufuatia hayo alitishia kubomoa nyumba ambayo alikuwa amemjengea.

"Sawa, haina shida. Nilikuwa nataka tu kujua msimamo wako. Hata nyumba nilikujengea nitabomoa nijenge nyingine. Inakaa ikifanya nini? Acha nitajenga nyingine yangu hapo kando," alisema Sammy.

Je, Ungewashauri vipi wawili hao?