Maelezo: Fahamu kwa nini hakutakuwa na Patanisho wiki hii

Mashabiki watafurahia kupeperushwa tena kwa Patanisho bora zilizopeperushwa katika miaka ya hivi majuzi.

Muhtasari

•Hali hiyo inatokana na kutokuwepo kwa mtangazaji mkuu wa kipindi hicho cha asubuhi, Gidi Ogidi ambaye yuko likizoni.

•Mashabikiwataendelea kufurahia upeperushaji wa Patanisho kuanzia wiki ijayo kwani Gidi atakuwa amerejea studioni.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Mamilioni ya mashabiki wa Patanisho katika kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo hawataweza kufurahia upeperushaji wa moja kwa moja wa kitengo hicho maarufu juma hili, Septemba 4- Septemba 8.

Hata hivyo, ndani ya kipindi hicho watapata kufurahia kupeperushwa tena kwa Patanisho bora zaidi ambazo vimepeperushwa katika miaka ya hivi majuzi.

Kutokuwa na vipindi vya moja kwa moja vya Patanisho kunatokana na kutokuwepo kwa mtangazaji mkuu wa kipindi cha asubuhi, Gidi Ogidi ambaye yuko likizoni.

“Patanisho bado ipo. Lakini nitakachofanya, nitacheza ‘Best of Patanisho’ alafu tuweze kutoa maoni yetu pale,” Ghost Mulee alitangaza siku ya Jumatatu asubuhi wakati wa kipindi.

Mtangazaji huyo mahiri aliongeza, “Patanisho huwa na matukio tofauti na huwa tunakusanya ‘best of Patanisho’ tunakuwekea alafu tutakuwa tukijadiliana baada ya kusikiliza.”

Gidi ambaye anaongoza kipindi maarufu cha Gidi na Ghost Asubuhi kinachopendwa na mamilioni ya mashabiki hatakuwa hewani kwa muda wote wa wiki hii.

Aliondoka nchini kuelekea Uingereza siku ya Ijumaa ambako alishuhudia moja kwa moja mechi ya Arsenal dhidi ya Manchester United kwenye uwanja wa Emirates siku ya Jumapili jioni. Baada ya kutazama mechi hiyo ambapo timu yake pendwa ya Arsenal iliwanyorosha wapinzani wao wa siku bila huruma, Gidi alieleza kuwa ni hisia bora kuwahi kutokea.

"Hisia Bora zaidi kuwahi kutokea. Mancheter United 1, Arsenal 3.. hisia bora kabisa. Gunners, Arsenali. Mambo ni matatu,” alisema.

Mtayarishaji wa kipindi, Martin Njoroge Kiptoo hata hivyo amewahakikishia mashabiki kwamba wataendelea kufurahia utangazaji wa moja kwa moja wa kitengo wanachokipenda zaidi cha Patanisho kuanzia wiki ijayo kwani Gidi atakuwa amerejea studioni.

“Wiki hii hatutafanya Patanisho kwani Gidi yuko nje ya Nchi. Hatakuwepo wiki hii nzima. Wiki hii tutacheza ''Bora zaidi ya Patanisho '' ambayo imeonyeshwa katika miaka iliyopita...," Martin alisema.

Jumatatu asubuhi, Radio Jambo ilipeperusha tena Patanisho kutoka Januari 2021 ambapo Daniel Musamali aliomba apatanishwe na mama mkwe wake, Mama Dina.

Kipindi hicho kilikuwa na mvutano mkubwa kwani Daniel na mama mkwe wake hawakuweza kukubaliana hata kidogo. Hatimaye Gidi alimshauri kijana huyo kumpa Mama Dina muda wa kutulia kabla wajaribu tena kusuluhisha mzozo wao.