Mambo imechemka! Wafula achanganyikiwa baada ya mkewe kuapa kurudi kwa lazima na kufukuza atakayepata nyumbani

"Nimeona bado ako na speed ingine. Nilikuwa nampima tu. Mimi sina mke," Wafula alisema.

Muhtasari

•Ruth alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika Aprili mwaka huu baada ya mumewe kumuacha nyumbani miezi mitatu.

•Matamshi ya Ruth yalionekana kugeuza ghafla msimamo wa Wafula na akakiri kuwa alikuwa anafanya mzaha tu akisema ako na mke mwingine.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho kwenye Gidi na Ghost Asubuhi, mwanadada aliyejitambulisha kama Ruth Sarfu ,24, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Wafula ,26, ambaye amezaa naye mtoto mmoja.

Ruth alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika Aprili mwaka huu baada ya mumewe kumuacha nyumbani miezi mitatu.

Alisema Wafula alikosa kumshughulikia na mtoto wao wakati walipougua, jambo lililopelekea yeye kutoroka.

"Mwezi wa nne nilikuwa kwa boma ya mume wangu akaniacha miezi mitatu. Nikampigia simu nikamwambia mtoto ni mgonjwa, akasema. Jirani akanipa dawa, nikapea mtoto akapona. Nami nikawa mgonjwa, nikampigia simu hakuchukua. Mama yake akanipeleka hospitali nikalazwa wiki moja," Ruth alisema.

Aliendelea, "Wakati nilipona, aliniuliza kama nimepata nguvu ya kuenda kwetu. Nilifika mahali nikaona nirudi kwa wazazi wangu. Nilitoka saa nane usiku, nikachukua kila kitu yangu tukaenda. Hapo mwanzoni tulikuwa tunazungumza kwa simu ikafika mahali nikimpigia simu ananiambia ataniita. Nikiwa mgonjwa aliniambia, "Wewe ukitaka kufa niko na ujuzi wa kuchimba kaburi ya corner nne". Huwa ananipigia tu simu lakini hajakuja kwetu. Mimi bado nampenda. Nilikuwa nampenda na roho moja."

Ruth alisisitiza kuwa licha ya yaliyotokea, bado anampenda sana mume wake na kusema angependa kujua msimamo wake.

Wafula alipopigiwa simu alibainisha kuwa hakumfukuza mkewe bali uamuzi wa kugura ndoa yao ulikuwa wake.

Hata hivyo, alifichua kuwa alijitenga na Ruth miezi mitatu kwa makusudi kwani alitaka achukue hatua ya kuenda mwenyewe.

"Mwanamke akifanya uamuzi wake unamuacha afanye kwanza. Mimi nilimuacha afanye maamuzi yake," Wafula alisema.

Aliendelea, "Yeye ako na tabia mbaya. Kwa boma haelewani na watu. Alikuwa anaanza kutusi tusi mama yangu nikasema nimpatie punishment. Na mama alimpeleka hospitali vizuri. Sikumfukuza, yeye alitoroka tu. Mimi nilitoroka kwa boma afanye vile anataka. Yeye anataka awe juu zaidi. Lakini kama amekaa chini na akaona makosa yake pia ni sawa."

Katika utetezi wake, Ruth alisema, "Najua nilikosa kutoka kwa boma bila idhini yako. Lakini ni wewe mwenyewe ulifanya nitoke. Kuniacha kwa nyumba miezi mitatu bila chochote. Mimi naona sina makosa yoyote, isipokuwa ndugu yako mdogo alinishikia mwiko akitaka kunipiga. Sikubishana naye nilienda nikajifungia kwa nyumba.Sijawahi kutusi mamako.  "

Wafula alilalamika kuwa mama mkwe wake aliwahi kumtusi vibaya, jambo ambalo liliongeza hasira ndani yake.

Wakati huo huo, alidai kuwa tayari ameoa mke mwingine na kusema Ruth yuko huru kurudi ikiwa atakubali kuwa mke wa pili.

"Nitakwambia wakati utarudi mimi mwenyewe. Unaniharakisha aje?.. Kusema ukweli nilioa. Nilipata mwanamke mwingine. Mtu kama hanielewi itakuwaje? Acha arudi akuwe mke wa pili. Kama atakubali mimi niko tayari basi," alisema.

Ruth alisema, "Kulingana na kabila hatuwezi kaa wawili. Sisi huwa tunabaki tu mmoja na huwezi kuongezwa mwenzako.

Alimwambia Wafula, "Nashukuru sana kwa wewe kupata mke mwingine,  lakini usimtese vile ulinitesa. Mkae naye mzae watoto mlee. Nilitaka kujua tu msimamo wako. Sasa nimejua na nitajipanga.

Matamshi ya Ruth yalionekana kugeuza ghafla msimamo wa Wafula na akakiri kuwa alikuwa anafanya mzaha tu akisema ako na mke mwingine.

"Nimeona bado ako na speed ingine. Nilikuwa nampima tu. Mimi sina mke," alisema.

Kufuatia hayo, Ruth aliweka wazi kuwa tayari amejipanga kurudi na kuapa kufukuza yeyote ambaye atapata kwa nyumba.

"Mimi nimepanga vitu. Naanza safari saa hii. Mimi ndio naingia hapo. Mimi ndio bibi yako milele na milele. Nachukua boda na yeye ndiye atalipa," alisema.

Wafula alisema, "Hii mambo imechemka. Unarudi lakini usirudi leo. Nitakwambia."