"Nilidhani ni Mmeru!" Mwanamke ashangaa baada ya mamake kumweleza ukweli kuhusu baba yake Mkisii

Millicent hajazungumza na mamake katika miaka 10 iliyopita baada ya kumtusi vibaya kwa kutomwambia babake halisi ni nani.

Muhtasari

•Millicent alikiri kwamba hajaweza kukutana na mzazi huyo wake wala kuzungumza naye katika miaka kumi iliyopita.

•Mamake Milicent hata hivyo alikubali kumwambia ukweli binti yake kutokana na hatua yake ya kuomba msamaha.

Image: RADIO JAMBO

Mwanadada aliyejitambulisha kama Millicent Barut ,35, kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake mzazi Jane Kagendo ,55, ambaye alikosana naye takriban mwongo mmoja uliopita.

Millicent alikiri kwamba hajaweza kukutana na mzazi huyo wake wala kuzungumza naye katika miaka kumi iliyopita baada ya wao kukosana miaka kumi iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Alisema uhusiano wake na mamake ulivunjika wakati alipomtusi baada ya kukataa kumwambia baba mzazi wake ni nani.

"Nilimuuliza baba yangu mzazi ni nani akakataa kuniambia. Hapo ndo tukakosana. Miaka kumi sijawahi kutana na mamangu na ata hatujawahi kuongea. Hajawahi kunitafuta. Niliamua kuolewa," Millicent alisema.

Aliongeza, "Dada zangu huwa wananiongelesha. Mimi ni wa nje, wengine ni wa baba wa kambo. Kulikuwa na shangazi yangu mmoja, sijawahi kumuuliza lakini. Nilitaka kumuuliza lakini nikasema ningoje kwanza."

Millicent alipoulizwa sababu ya kutaka kumjua babake mzazi, alisema "Baba wa kambo hakuwahi kunipenda kabisa. Baada ya kuzaliwa mtoto wake wa kwanza kijana, alianza kunipiga. Niliishi kusema nikipata mahali ya kuenda naweza kuenda.Hata mtu ambaye alinioa alikuwa mgeni kwa ile ploti nilikuwa naishi.

Aliona yale nilikuwa napitia akaniuliza kama naweza kubali kuishi na yeye. Nilimwambia nifanye mtihani wa darasa la nane kwanza. Nilipofanya mtihani nilichelewa kuenda nyumbani alafu nikapigwa sana. Hapo ndio niliamua kutoka. Hata huku kwa ndoa napitia mengi tu, nasema heri ningetafuta kazi."

Mwanadada huyo alikiri kwamba alimtupia mamake cheche za maneno makali, akimkosoa kwa kutomwambia babake.

Bi Jane alipopigiwa simu, bintiye alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha.

"Ningependa kukuomba msamaha kwa maneno yenye nilikuambia. Nilikutusi vibaya lakini ningependa unisamehe. Inanifuata tu," Millicent alimwambia mamake.

Bi Jane alisema, "Ni sawa nitakusamehe lakini si unajua vile ulinitusi vibaya.. Nimemsamehe lakini alinitusi vibaya. Alikuwa anataka kujua baba ambaye alimzaa lakini nikakataa akanitusi vibaya."

Alipoulizwa sababu ya kukataa kumwambia bintiye baba yake ni nani, Bi Jane alisema "Sikutaka kumwambia kwa sababu nilikuwa kwa mwingine, na huyo mwingine ndiye alimlea kama baba yake. Nikaona akae na huyo."

Mamake Milicent hata hivyo alikubali kumwambia ukweli binti yake kutokana na hatua yake ya kuomba msamaha.

"Vile anataka kujua huyo baba yake, na kwa vile ameomba msamaha nitamwelezea. Namfahamu baba yake mahali ako, na mimi nimekaa miaka mingi bila kuongea na yeye. Sina ata namba yake, sasa nashindwa nitamweleza aje huyo mtoto.

Lakini sasa atamjua aje lakini sina namba yake ya simu. Anaitwa Peter Gesora, anatoka Keroka. Alikuwa anakaa na ndugu yake Omiti ambaye alikuwa mwanajeshi,"  Jane alisema.

Millicent alisema "Ata sikuwa najua baba ni Mkisii. Nilikuwa najua babangu ni Mmeru. Nimeridhika na nimeshukuru sana."

Alimwambia mamake, "Nimesema asante, ata naskia roho yangu niko sawa kabisa. Hakuna mama mwingine ni wewe tu."

Bi Jane alisema, "Ni sawa tu nimemsamehe. Ajue mzazi ni mzazi."