"Nilipata baba alikufa na kuzikwa" Mwanadada azozana na mamake kwa kumzuia kuwa na babake

Felista alidai walipata baba yake alizikwa miaka miwili iliyopita, mamake hakuwa na habari.

Muhtasari

•Felista alieleza kuwa ugomvi na mama yake ulianza pale aliposisitiza kuwa anataka kumuona babake mzazi ambaye hakuwa ameambiwa kumhusu mapema maishani.

•Bi Judith alibainisha kwamba hakufurahishwa na jinsi bintiye alivyomuongelesha na kufichua mengi zaidi kumhusu.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Mtangazaji Jacob Ghost Mulee ndani ya studio za Radio Jambo.

Katika kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Felista Sakwa (30) kutoka Kapsabet alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake Judith.

Felista alifichua kwamba uhusiano wake mzazi huyo wake ulivunjika mwezi Desemba mwaka jana baada ya yeye kumkosea heshima na kumuongelesha isivyofaa.

Alieleza kuwa ugomvi na mama yake ulianza pale aliposisitiza kuwa anataka kumuona babake mzazi ambaye hakuwa ameambiwa kumhusu mapema maishani.

"Toka nikiwa mdogo, mama yangu hakunieleza kuwa nina babangu mzazi ambaye sio mwenye alinilea. Wakati moja nilienda matanga Western. Mzee fulani akaniita kwa jina la nyumbani, nikamuuliza alinijua aje na sijawahi kuenda huko.. Aliniambia ni babangu na anataka tuende nyumbani tukae huko," Felista alisimulia.

Felista alidai hata hivyo mama yake alimkataza kuenda na mwanaume  huyo aliyedai kuwa mama yake.

Alifichua zaidi kuwa baba yake alimfuatilia baadaye alipojiunga na shule ya upili.

"Nilkiwa na miaka kama minane, alikuja kama mara  tatu kunitafuta. Nikiwa shule alikuwa ananifuatilia. Alikuja akaniambia angependa sana tuende na yeye. Lakini kwa jinsi mama yangu alikatakaa, aliniambia kwaheri ya kuonana na kusema ningekuja kumtafuta baadaye, niliskia uchungu sana," alisema.

Felista pia alifunguka kuhusu wakati mzozo ulitimbuka baina yake na mamake akisema,"Wakati nikiwa mkubwa nikamuuliza yule mzee alikuwa ananipigania nikiwa mkubwa ni nani? Akasema ni babangu alikosana naye wakati akiwa mjamzito,

Tulipata matanga tena huko nyumbani, nikasema naenda na yeye. Tulipotaka kuenda, nikamwambia mamangu nataka kujua familia yangu. Mama akakataa. Shangazi wangu walimsihi akubali. Kufika kule tukapata babangu alishakufa na akazikwa, mama hakuwa na habari. Hiyo ndiyo ilifanya nikosane naye."

Hata hivyo alidai anajuta jinsi alivyomuongelesha mzazi huyo wake na hivyo akasema anataka kumuomba msamaha.

"Nilimuongelesha lakini hakuwa na ile roho ya kuomba msamaha," alisema.

Bi Judith alipopigiwa simu, Felista alichukua fursa kumuomba msamaha huku akisikika mwenye majuto na uchungu.

"Mama naomba unisamehe vile nilikuongelesha ile siku, ni hasira. Nitakuja nyumbani ila nisamehe tu. Najuta kukuongelesha vile na jinsi umepita hali ngumu na mimi," alisema.

Bi Judith aliweka wazi kwamba yuko tayari kumsamahe bintiye ila akamwagiza achukue hatua ya kurejea nyumbani.

Hata hivyo alibainisha kwamba hakufurahishwa na jinsi mtoto huyo wake alivyomuongelesha na kufichua mengi zaidi kumhusu.

"Akuje nyumbani tuongee. Alitoka hapa 2007 akapotea. Alipatikana ako jela. Nilishughulika kama mzazi. Huyo ametembea mpaka Tanzania na Burundi. Sijui vile walipelekana na mwingine huko Mombasa akapelekwa jela.

Nilimtafuta chifu akanisaidia nikampigia yule askari ambaye alikuwa amemfunga jela tukaongea na yeye. Aliniunganisha na mwanamke aliyekuwa amempeleka jela tukazungumza. Sikuwa nimemuona miaka 13," alisema.

Aliongeza, "Alikuja hapa nyumbani nikamuambia atulie. Kukaa kidogo akaenda mpaka Mombasa. Akawa mgonjwa. Akaniambia hana nauli, nikamtumia. Alipokuja nikamwambia atulie. Akawa haskii, anataka nimpatie pesa. Ndio huyo tena akaenda Nakuru. Nilimwambia kama anaona simsaidii atakuja kukumbuka."

Felista alikubali makosa yake na kumsihi mama yake amsamehe. Aliahidi kurudi nyumbani atakapopata nauli.